Chadema yampa tano Rais Samia

Muktasari:

  • Viongozi wa Chadema wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuruhusu mikutano ya hadhara, huku wakimtaka kuwavumilia pindi watakapomkosoa kwa hoja na sio matusi.

Mwanza. Viongozi wa Chadema wamesema watatumia mikutano ya hadhara kuwafikia wananchi kusikiliza kero zao pamoja na kufikisha ujumbe wao na sio matusi.

Wakitoa salamu kwa wananchi waliofika kwenye uzinduzi wa mikutano ya hadhara wa chama hicho viwanja vya furahisha jijini Mwanza leo Jumamosi, Januari 21, 2023 viongozi hao pia wamempomgeza Rais Samia Suluhu Hassan kuruhusu mikutano hiyo.

Aliyeanza kutoa salamu ni Spika Kivuli wa Bungela Wananchi Chadema, Suzan Lymo aliyesema kila mbunge na diwani kivuli atakwenda kuangalia kero katika eneo lake pamoja na kuishauri na kusimamia Serikali.

“Kwahiyo kwakufanya hivyo tunawatetea japo hatupo Dodoma,” amesema.

Mbunge wazamani waMbeya mjini,Joseph Mbilinyi (Sugu) amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuruhusu mikutano ya hadhara akisema wanazo hoja za kuongea na wananchi.

“Ninayo furaha kuwa hapa na nampongeza Rais kwa kuwa na ujasiri wa kukubari kuondoa zuio haramu la mikutano ya hadhara kwa miaka saba.

“Hoja tunazo hali ni tete, hali ni ngumu, wananchi wamechoka sana, hakuna anayewasemea ipasavyo,” amesema

Amesema kupitia mikutano ya hadhara wataenda kila sehemu kuzungumzia changamoto za maji, umeme na hali ngumu ya maisha inayowakumba wananchi.

Naye Katibu wa Baraza la wanawake Chadema Taifa, Catherine Ruge amesema licha ya kuwa katika kifungo cha kisiasa kwa miaka saba kimewaimarisha na kuwapa nguvu mpya.

“Kwetu sisi wanawake wa Chadema miaka saba imekuwa chuo cha mafunzo na ujasiri na sasa imetuimarisha, tumeimarika na tupo tayari kuwamsitari wa mbele kuongoza mapambano, jukumu la wanawake wa Chadema ni kuibua kero za wananchi wetu,” amesema

Amesema wanatamani kuona jamii, wanawake na watoto wanapata huduma bora.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Grace Kiwelu amemuhakikishia Rais Samia kuwa chama hicho hakitotumia majukwaa ya mikutano ya hadhara kutukana matusi badala yake watatoa hoja.

Mwenyekiti wa Baraza la wazee wa Chadema, Hashimu Issa Juma amesema licha ya Rais Samia kuwaheshimisha wanawake wa Tanzania lakini itambidi avumilie chama hicho kumkosoa.

Ameipinga kauli ya Rais Samia ya kuwa Serikali imeandaa mazingira bora ya vijana kujiajiri akidai hakuna mazingira bora huku akimtaka aondoe sheria ya uhujumu uchumi kuvutia wawekezaji.

“Serikali inajukumu la kupatia vijana ajira na ndivyo dunia nzima inavyofanya,” amesema

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema, John Pambalu ameiomba Serikali kukaa pamoja kupitia meza ya mazungumzo kuwarudisha wamachinga kufanya biashara zao.