Chakamwata waiangukia Serikali kuingilia kati kupewa zuio

Muktasari:

  • Chakamwata waiomba Serikali kuingilia kati zuio lililotolewa na msajili wa vyama vya wafanyakazi na ajira, ili waweze kuendelea na shughuli za chama hicho.

Dar es Salaam. Chama cha Kutetea Haki na Maslahi ya Walimu Tanzania (Chakamwata) waiomba Serikali kumwambia Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Ajira atengue zuio la mkutano wao ili wajadili hatima ya chama hicho.

Ombi ambalo wanahitaji kwa sasa  ni kuruhusiwa kufanya mkutano kwani chama chao kipo kisheria tangu mwaka 2015 ili waweze  kujadili mustakabali wa chama ikiwepo matumizi ya fedha, uwazi na namna ya kuhudumia wanachama wao.

Akizungumza na Mwananchi leo Mei 26 Kaimu Mwenyekiti Ashery Ntagomora amesema uamuzi wa kusimamisha shughuli za chama na kuzuiwa kwa akaunti ya chama  hicho ni pigo kwa walimu ambao ni wanachama.

Ofisi ya msajili ilifikia hatua hiyo wakati chama kikiwa katika maandalizi ya kufanya mkutano mkuu ambao ulikuwa na ajenda ya kuidhinisha bodi ya wadhamini na malengo ya chama hicho.

Kwa mujibu wa barua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Ajira yenye namba ya kumbukumbu RTU/U/194/02/49, iliyoandikwa Julai 30, 2019 kwenda kwa mwenyekiti wa chama hicho ikiwaeleza kusudio la ofisi hiyo kuzuia mkutano huo mkuu wa taifa.

Barua hiyo iliyosainiwa na Kaimu Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Ajira, Pendo Berege, ilieleza kuwa ofisi yake ilipata taarifa za kuitishwa kwa mkutano ngazi ya taifa  hivyo chama hicho hakijasajili bodi ya wadhamini.

"Tulimtumia mwaliko wa mkutano mkuu pamoja na nyaraka zetu za chama na malengo makuu ya mkutano huo lakini tulipopokea barua ya kusitishwa kwa mkutano wetu hatukuelewa tumekosea wapi," alisema Ntagomora.

Alidai kuwa kwa sasa kumeshakuwa na matukio mengi ambayo kama chama ilishajipangia vya kufanya lakini wanashindwa kufanya chochote kwa sababu akaunti za chama zimezuiwa.

"Hii yote imetokana na hujuma za aliyekuwa katibu wa chama hicho Meshack Kapange kwa matakwa yake tu na kwa kuwa anafahamiana na baadhi ya watu hivyo anapata nguvu ya kuhujumu chama chetu," alisema.

Kutokana na kinachoendelea anasema kadhaa wameenda mpaka Ikulu na kuzunguka katika sekta tofauti za serikali ili kusaidiwa katika kutetea maslahi ya chama chao.