Chama cha ushirika Nyanza charejeshewa mali ya Sh20 bilioni

Chama cha ushirika Nyanza charejeshewa mali ya Sh20 bilioni

Muktasari:

  • Chama kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza (NCU) kimerejeshewa mali zake za Sh20 bilioni zilizohodhiwa na watu binafsi waliouziwa kinyume cha sheria.

Mwanza. Chama kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza (NCU) kimerejeshewa mali zake za Sh20 bilioni zilizohodhiwa na watu binafsi waliouziwa kinyume cha sheria.

Kaimu meneja mkuu wa NCU, Martha Ndetto ametaja mali hizo kuwa ni majengo, viwanja, ghala, kituo cha mafuta na karakana vilivyoko maeneo mbalimbali jijini Mwanza.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa 29 wa chama hicho jijini Mwanza leo Jumatatu Machi 29, 2021, Ndetto amesema tayari NCU imekabidhiwa hati saba kati ya nane za mali zilizorejeshwa.

“Taratibu za kisheria zinaendelea kuwezesha kupatikana na kukabidhiwa kwa hati ya mali ya nane ambayo imegundulika aliyeuziwa aliiweka dhamana ya mkopo benki.”

“Kurejeshwa kwa mali hizo kumeiwezesha NCU kutengeneza faida ya zaidi ya Sh1 bilioni kutokana na pango, fedha anazosema hazitumiki bila kupata ridhaa ya uongozi wa Serikali,” amesema Ndetto.

Mwenyekiti wa NCU, Benjamini Mikomangwa amesema uongozi wa chama unatarajia kuomba idhini ya wanachama kutumia fedha hizo kwa ajili ya ukarabati wa majengo yake kwa lengo la kuyaongezea thamani itakayowezesha malipo na faida zaidi itakayosaidia kulipa deni la kodi inayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Akizungumza na wajumbe wa mkutano huo ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza, Maua Ally amewataka wanachama wa NCU kutimiza wajibu wa kutunza na kulinda mali za ushirika kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.

Kuhusu uchaguzi wa viongozi wapya ambayo ni moja ya ajenda za mkutano huo, Maua amesema Takukuru inafuatilia kwa karibu nyendo za wagombea na wajumbe kudhibiti vitendo vya rushwa.