Changamoto kwa mawaziri wapya

Muktasari:

  • Mawaziri wanne wapya na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), walioapishwa juzi na Rais Samia Suluhu Hassan, wanasubiriwa na changamoto ambazo zinatajwa kuwakwaza wananchi huku Wizara ya Nishati ikiongoza.


Moshi. Mawaziri wanne wapya na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), walioapishwa juzi na Rais Samia Suluhu Hassan, wanasubiriwa na changamoto ambazo zinatajwa kuwakwaza wananchi huku Wizara ya Nishati ikiongoza.

Katika uteuzi alioufanya usiku Septemba 12, Rais alimteua Januari Makamba kuwa Waziri wa Nishati kuchukua nafasi ya Dk Medard Kalemani na Profesa Makame Mbarawa kuwa waziri mpya wa ujenzi.

Dk Stergomena Tax aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa Teknolojia, Habari na Mawasiliano (Tehama) na Jaji Eliezer Feleshi kuwa AG mpya wa Serikali.

Hata hivyo, gazeti la Mwananchi lilizungumza na wadau mbalimbali na kuainisha changamoto wanazoamini zinahitaji kuangaliwa kwa jicho la kipekee na Serikali.

Dk Tax ambaye ni mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Ulinzi tangu Tanzania ijipatie uhuru wake mwaka 1961, anachukua nafasi ya Elias Kwandikwa, aliyefariki Agosti 2021 wakati Profesa Mbarawa akichukua nafasi ya Dk Leonard Chamuriho.

Zigo la Waziri Makamba

Waziri Makamba, aliyewahi kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne na Tano, anakabiliwa na changamoto ya utitiri wa tozo katika nishati ya mafuta ambayo imesababisha bei kuwa juu na kuumiza wananchi. Mapema mwezi huu Serikali ilizuia kupanda kwa bei ya mafuta huku ikiunda timu kuchunguza na kuangalia viashiria vinavyofanya kupanda kwa bei.

Takwimu zinaonyesha katika kipindi cha mwaka mmoja bei ya petroli na dizeli imepanda kwa zaidi ya Sh885 kutokana na ongezeko la bei katika soko la duniani, kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na mabadiliko ya tozo mbalimbali.

Waziri wa Nishati, Januari Makamba 

Juni mwaka jana, bei ya mafuta mkoani Dar es Salaam ilishuka hadi Sh1,520 kwa lita moja ya petroli, dizeli Sh1,546 na mafuta ya taa Sh1,568, kwa sasa lita moja ya petroli ni Sh2427.

Pia, Makamba atakumbana na changamoto ya kupanda kwa bei ya umeme na gesi za majumbani iliyotokana na kuanzishwa kwa tozo ya majengo kupitia ununuzi wa umeme. Hata hivyo, changamoto hiyo imekuwa ikihusisha wizara zaidi ya moja huku ufumbuzi wake ukiendelea kupatiwa majibu.

Waziri huyo atakumbana na kero kubwa ya kukatika umeme maeneo mengi ya nchi na uunganishaji wa huduma hiyo kupitia Mamlaka ya Umeme Vijijini (Rea).

Pia, anakabiliwa na changamoto ya kusukuma mpango wa Serikali wa kubadilisha mifumo ya magari kutoka kutumia mafuta, nishati ya gesi na mbadala ili kuokoa mazingira. Akiwa Waziri wa Mazingira, Januari alisifika kwa kusimamia vyema agizo la kusitishwa kwa matumizi ya mifuko ya plastiki isiyokidhi viwango stahiki.

Waziri wa Ujenzi

Katika Wizara ya Ujenzi kuna miradi mikubwa iliyoanzishwa na Serikali chini ya Hayati John Magufuli, ukiwamo wa treni ya kisasa (SGR), hivyo Profesa Mbarawa ana kibarua cha kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Kibarua hicho kinatokana na ukweli kuwa mradi huo unatumia fedha nyingi za walipa kodi na Watanzania walielezwa kuwa treni ya majaribio ingeanza Juni mwaka huu, lakini inaonekana kusogezwa hadi Desemba. Kwa mujibu wa Shirika la Reli (TRC) ujenzi wa reli ya kisasa unaendelea ambapo, kipande cha kwanza kati ya Dar es Salaam na Morogoro kilichoanza kujengwa Mei 2, 2017 umekamilika kwa asilimia 100 na majaribio ya treni yanatarajiwa kuanza Novemba, mwaka huu.

Profesa Mbarawa

Changamoto nyingine ni malalamiko kuhusu ubora wa barabara za lami zinazojengwa nchini. Profesa Mbarawa atatakiwa kuboresha viwanja vya ndege na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ambalo kwa siku za karibuni linalalamikiwa kuwa na nauli bei juu na kuahirishwa safari mara kwa mara pamoja na kujiendesha kwa hasara licha ya Serikali kufanya uwekezaji mkubwa.

Kwa sasa ATC inamiliki ndege za kisasa ikiwemo Airbus, Dreamliner na Bombadiar ambazo hata hivyo hazijaweza kulikwamua shirika hilo kutoka kwenye hali mbaya kiuchumi huku ikiwa na mzigo mkubwa wa madeni.

AG na Waziri wa Ulinzi

Mwanasheria Feleshi anaonekana kuguswa na changamoto nyingi zinazohusu maboresho ya sheria zinazolalamikiwa na wadau, ikiwamo ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 inayomgusa Dk Kijaji.

Mbali na sheria hiyo, zipo sheria zilizopitishwa na Bunge zikianzia katika ofisi yake zinazolalamikiwa na mojawapo ni sheria inayowapa nguvu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi kwa wakulima wa tumbaku.

Changamoto kwa mawaziri wapya

Hili lilimfanya Spika wa Bunge, Job Ndugai akatishia kuifumua Kamati ya Bunge ya Bajeti kwa kuruhusu bajeti hiyo, lakini baadaye kamati ilieleza kuwa hata wao waliipinga, lakini Serikali ilishikilia msimamo bungeni hadi ikapita.

Dk Kijaji na sekta ya habari

Wadau wa tasnia ya habari wanasema Dk Kijaji anakabiliwa na changamoto kubwa ya uwapo wa sheria kandamizi za uhuru wa habari nchini.

Mwenyekiti wa Misa-Tanzania, Salome Kitomari alisema kwa muda mrefu wadau wamepigia kelele dosari zilizopo katika sheria zinazosimamia sekta ya habari na anatamani Waziri Kijaji angekuja na suluhisho la changamoto hiyo.

“Misa tumefanya uchambuzi wa sheria ya huduma za vyombo vya habari tukaainisha maeneo muhimu yanayopaswa kufanyiwa mabadiliko ili kuondoa migongano iliyojitokeza,” alisema Kitomari.

Waziri wa Teknolojia, Habari na Mawasiliano (Tehama), Dk Ashatu Kijaji

“Hivi karibuni gazeti la Raia Mwema lilifungiwa, lakini ukiangalia utetezi wao wala haukuzingatiwa kwa sababu katika ile hukumu tungeona hata wao wamesema nini,” alisema Kitomari.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alisema waziri anapaswa kuanza na mabadiliko ya sheria, hasa kanuni ambayo Serikali anakuwa mlalamikaji, mwendesha mashtaka na mtoa hukumu wa kesi inayomhusu.

“Kwa hiyo kifungu kile cha 9(b) cha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kinapaswa kuondolewa kwenye hiyo sheria tukabaki na kifungu cha 52 kinachotaka walalamikaji kwenda mahakamani,” alisema Balile.

Balile alimtaka waziri kuhakikisha mfuko Wakfu wa Vyombo vya Habari unatengewa angalau Sh5 bilioni na Serikali ili kusomesha wanahabari na akataka kuwepo kwa chombo kimoja kinachosimamia wanahabari badala ya utitiri.

“Mfuko wa vyombo vya habari hauna chanzo cha mapato. Kutegemea wamiliki wa vyombo vya habari kwamba ndio watachangia wakati wako hoi hawajalipa mishahara hawajafanya nini haiwezekani kusubiri wafadhili.”

Mwenyekiti wa Klabu ya Wanahabari Mkoa Kilimanjaro (Mecki), Bahati Nyakiraria alisema kama angekutana na waziri, angemsihi aanze kuondoa vipengele vya Sheria ya Huduma za Habari vinavyozuia uhuru wa habari.

Wananchi, wasomi wafunguka

Mwenyekiti wa Tanganyika Law Society (TLS) Kilimanjaro, David Shillatu alisema Waziri wa Habari, Dk Kijaji anakabiliwa na changamoto ya kuhakikisha uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza unatamalaki nchini.

“Ni lazima asahihishe makosa na sheria zinazokandamiza uhuru wa habari. Wadau wamepiga kelele sana. Hii kufungia fungia magazeti haina afya. Waache vyombo vya habari vitekeleze wajibu wake. Hapo Kenya tu wanatushinda,” alisema.

Kuhusu Wizara ya Ulinzi, Shillatu ambaye ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, alisema waziri anakabiliwa na changamoto ya ulinzi mikoa ya kusini kutokana na vitisho vya magaidi walioko Msumbiji ambao huleta chokochoko nchini.

Kuhusu Wizara ya Nishati, Shillatu alisema suala la tozo kwenye mafuta ni jambo linalopigiwa kelele sana na Watanzania akisema bei ya petroli na Diesel kwa Tanzania iko juu kuliko nchi jirani wakati soko la dunia ni moja.

Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kilimanjaro, Basil Lema alisema mawaziri hao wanakabiliwa na changamoto ya kuwarudishia furaha Watanzania kutokana na mzigo wa tozo na kodi.