Chanzo kifo cha Mtanzania mwenye digrii saba chatajwa

Profesa Handely Mwafwenga enzi za uhai wake.
What you need to know:
- Profesa Mwafwenga amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, Septemba 19, 2023 wakati akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Afisa Usimamizi wa Fedha Mkuu Daraja la Kwanza wa Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Profesa Handely Mafwenga amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.
Mafwenga alikuwa na shahada saba, kati ya hizo, moja ikiwa ni shahada ya awali (BA), huku shahada za uzamili (Masters) zikiwa tatu, na kwa shahada uzamivu (PhD), alikuwa nazo tatu pia.
Imeelezwa kuwa Profesa Mafwenga amefariki usiku wa kuamkia leo 19, 2023, wakati akipatiwa matibabu ya figo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.
Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na familia yake kupitia kwa mdogo wake, Innocent Mafwenga ameeleza kuwa Profesa Handely ambaye ni kaka yake alifariki majira ya saa saba usiku.
“Jana alikuwa amezidiwa ghafla na alipelekwa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) na tulipoenda asubuhi ya leo tumemkuta ameshafariki,”amesema Innocent.
Innocent amesema Profesa Mafwenga kwa muda mrefu alikuwa anasumbuliwa na tatizo hilo japo haikufahamika lakini baada ya kupima ikabainika kwamba anachangamoto ya figo.
“Mwanzoni alikuwa hajagundulika alikuwa anaumwa lakini tulikuwa hatujui kama ni figo lakini baadaye baada ya kupima ikagundulika na figo na alianza kudhohofika kwa kipindi kama cha mwaka mmoja hivi,”amesema.
Innocent amesema kwa kipindi cha nyuma muda mwingi alikuwa analalamika matatizo ya mgongo lakini baada ya kuona tatizo hilo linazidi ndipo alipenda hospitali na kubainika anatatizo hilo.
Hata hivyo, Wizara ya Fedha kupitia kwa Katibu Mkuu, Dk Natu Mwamba imetoa pole kwa watumishi, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu kwa msiba huo.
Innocent amebainisha kuwa Profesa Mafwenga aliyewai kuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameacha familia ya watu wa tano, mke na watoto wa nne.
“Watoto wake wote ni wakubwa kuna ambao wameshamaliza elimu ngazi ya vyuo na kuna baadhi wapo kazini,”amesema.
Kuhusu msiba, amesema unafanyika nyumbani kwake Mabwepande na keshokutwa wataanza safari kuelekea Tukuyu mkoani Mbeya kwa maziko.