Chongolo amaliza ziara Kilimanjaro, atoa maelekezo

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ametoa maelekezo kwa Serikali kufanya tathimini ya kiutendaji ya ukamilishwaji wa miradi yote inayosuasua ili kutekeleza ilani ya uchaguzi 2020/25 kwa ufanisi.


Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ametoa maelekezo kwa Serikali kufanya tathimini ya kiutendaji ya ukamilishwaji wa miradi yote inayosuasua ili kutekeleza ilani ya uchaguzi 2020/25 kwa ufanisi.

Akizungumza jana Jumamosi Agosti 6, 2022 wakati akihitimisha ziara yake ya siku nne mkoani Kilimanjaro, amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa miradi ya maji  ya Whona –Marangu –Omboni wa Rombo na ule wa Same –Mwanga –Korogwe inayopaswa kutatua kero ya huduma hiyo kwa wananchi.

“Nataka wizara ya maji kufanya kazi kwa bidi ili kutafsiri matokeo yaliyopo kwenye ilani, chama hakitawakalia kimya viongozi wasiotimiza wajibu wao kutatua changamoto zinazowakabili watanzania kwani huko ni sawa na kugombanisha chama na mwenyekiti kwa wananchi wake,” amesema  Chongolo.

Pia, Chongolo amesema hajaridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa barabara ya  Mwanga –Kikweni-Vuchama na kuagiza mamlaka zinazohusika kusimamia ujenzi huo, kuanza kumkata fedha mkandarasi anayejenga  kilomita 1.2 kwa kiwango cha lami endapo anatashindwa kukamilisha kwa wakati.

“Sisi tukiwacheleweshea mahitaji yao huwa wanatupa adhabu sasa kwa sababu sisi katika mradi huu hatujachelewesha ni wao wamezembea wapewe adhabu hiyo  na isiwe kigezo cha kuchelewesha huu mradi bali wakamilishe haraka ifikapo agosti 8 mwaka huu,” amesema

Chongolo ameziagiza wizara mbili Wizara ya Tawala na Mikoa  na Serikali za mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Fedha na Mipango kukamilisha ujenzi wa stendi  ya Ngangamfumani haraka iwezekanavyo inayotarajiwa kugharimu Sh17 bilioni hadi kukamilika kwake.

Chongolo ameagiza miradi yote inayotekelezwa kwa jamii, iwe imeibuliwa ngazi ya chini au vikao vya mashina mabalozi wanapaswa kushirikishwa kikamilifu ikiwemo kupokea maoni yao ili kufikia maamuzi kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi.