Chongolo ataka ruzuku kuwezesha uzalishaji wa mbolea

Friday May 13 2022
chongolopiic
By Noor Shija

Dodoma. Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ameagiza kuwa ruzuku itakayowekwa kwenye mbolea isaidie kuongeza uzalishaji wa ndani ili kulinda wawekezaji.

Chongolo amesema hayo Mei 13 alipotembelea kiwanda cha kuzalisha mbolea isiyo na kemikali cha Itracom Fertilizer LTD kilichopo jijini hapa ambacho mwekezaji wake ni raia wa Burundi.

“Wizara za Kilimo na Fedha wana maelekezo kutoka kwa Rais (Samia Suluhu Hassan) ya namna ya kutafuta mpango wa ruzuku kwenye mbolea. Maelekezo haya walipewa zaidi ya wiki tatu zilizopita,” amesema Chongolo.

Amesema lengo la Serikali ya CCM ni kuhakikisha yaliyotokea kwenye mbolea msimu wa kilimo uliopita hayajirudii.

Chongolo amesema mahitaji ya nchi ya mbolea ni tani laki saba na kiwanda hicho kinachotarajia kuanza uzalishaji Julai, kitazalisha tani laki mbili kwa awamu ya kwanza na kuwa na upungufu wa tani laki tano.

Amesema kutokana na hali hiyo Serikali ya CCM imeamua kutoa ruzuku kwenye mbolea kwa lengo la kuleta unafuu wa bei ya bidhaa hiyo kwa wakulima.

Advertisement

Msimu uliopita bei ya mbolea kwenye mikoa kama Iringa, Songwe, Ruvuma na Mbeya ilifikia mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya kukuzia kama UREA iliuzwa kwa Sh80,000 kutoka Sh50,000 waliokuwa wananunulia mwanzoni mwa mwaka 2021.

Pia, mbolea ya kupandia ya DAP iliyokuwa ikiuzwa kutoka Sh62,000 kwa mfuko wa kilo 50 na iliuzwa Sh90,000.

Mbolea nyingine zilizopanda bei ni mbolea za kukuzia aina ya SA ambayo mfuko wa kilo 50 uliuzwa Sh44,000 kutoka Sh38,000, mbolea ya CAN iliuzwa Sh55,000 kutoka Sh40,000 na mbolea ya NPK iliuzwa Sh90,000 kutoka Sh 60,000.

Chongolo amesema uamuzi wake wa kutembelea kiwanda hicho kumelenga kuanza kuratibu upatikanaji wa mapema wa mbolea na kwa bei nafuu.

Hata hivyo, alipoulizia bei ya mbolea ya kiwanda hicho alielezwa itauzwa kwa bei nafuu na itajulikana baada ya kuanza uzalishaji kwa kuwa mchakato unaendelea.

Naye meneja mradi wa kiwanda hicho, mhandisi Musafiri Dieudonue alisema ujenzi wa kiwanda hicho umefikia asilimia 80 na Julai kitaanza uzalishaji.

Amesema kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani laki sita za mbolea kwa mwaka na kitatoa ajira kwa watu 3,000. Kwa sasa wakati ujenzi ukiendelea kimetoa ajira 600.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesema kulikuwa na changamoto ya vibarua wazalendo kutokana na kazi ya upasuaji wa mawe na hivyo kulazimika kuleta vibarua kutoka Burundi.

Amesema kwa kuwa sheria za nchi haziruhusu vibarua wa kigeni walilazimika kutumia hekima na busara kuwezesha kuletwa kwa vibarua kutoka Burundi wenye uzoewefu wa upasuaji mawe na utendaji wenye ufanisi.

Kwa upande wake kamishna wa Uhamiaji jijini hapa, Bahati Jonathan alisema walifanikisha kuwezesha kiwanda hicho kuwa na vibarua kutoka Burundi na 143 wamekwisha pewa vibali vya kazi na wengine utaratibu unaendelea.Advertisement