Chongolo: Simamieni ubora mazao ya misitu

Katibu Mkuu wa CCM, Godfrey Chongolo akiwa ameambata na wajumbe mbalimbali wa ziara yake mkoani Iringa.

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo awataka wafanyabishara wa mazao ya misitu katika Wilaya ya Mufindi kusimamia ubora wa soko la mazao hayo.

Iringa. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amewashauri wafanyabishara wa mazao ya misitu kujenga utaratibu wa kuweka alama za utambuzi utakaotofautisha bidhaa zitokanazo na miti iliyokomaa na zile ambazo zimetokana na miti isiyokomaa.

Chongolo amesema hayo Mei 26, 2023 wakati alipopata nafasi ya kuzungumza na wafanyabiashara hao katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.

Mbali na wafanyabishara hao, Katibu Mkuu Chongolo alipata pia nafasi ya kuzungumza na viongozi wa dini pamoja na wazee wa mji huo.

Kiongozi huyo wa CCM alitoa ushauri huo baada ya mfanyabiashara Chesco Ng’umbi maarufu kwa jina la CF kuzungumzia utofauti wa bidhaa za misitu zinazotoka kwenye Shamba la Serikali la Saohill na mashamba ya watu binafsi.

Kulingana na wafanyabiashara, mbao na bidhaa nyingine za misitu zinazovunwa Saohill zimekomaa baada ya kukaa shambani kwa zaidi ya miaka 15 tofauti na zile zinazotoka kwenye mashamba binafsi ambazo huvunwa kuanzia miaka tisa.

Mufindi ni kati ya wilaya ambazo uchumi wake umebebwa kwa kiasi kikubwa na biashara ya mazao ya misitu, likiwemo shamba la Saohill.

“Mkijidanganya na mbao ambazo hazijakomaa mtaharibu soko, hili ni suala la ninyi kukubaliana.  Nimeona kwenye bidhaa za nguzo, wanaweka vibati ambavyo ukiona unajua hizi ni za wapi na zile za wapi, fanyeni hivyo na nyie,” ameshauri Chongolo.

Aliwashauri wafanyabishara hao kujiratibu na kuamua kuwa wamoja juu ya namna ya kusimamia ubora wa soko la mazao hayo ya misitu.

Awali, Diwani wa Mpanda ambaye pia ni mfanyabishara wa mazao ya misitu, Obadia Kalenga aliomba bei ya miti ya Serikali ishuke kutoka Sh80, 000 hadi 50,000.