Chonji na wenzake kortini kwa kusafirisha heroin, cocaine

Mshtakiwa Muharami Abdallah maarufu kama Chonji mwenye flana na karatasi mkononi akiwa na wenzake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumannne

Muktasari:

Mfanyabiashara anayefahamika kwa jina la Muharami Abdallah maarufu kama Chonji na wenzake wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin na cocaine zenye na thamani ya zaidi ya Sh328 milioni.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara anayefahamika kwa jina la Muharami Abdallah maarufu kama Chonji na wenzake wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini hapa, wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin na cocaine zenye uzito wa gramu 6203.85, zikiwa na thamani ya zaidi ya Sh328 milioni.

Washtakiwa hao wamepandisha mahakama hapo, leo Desemba 8, 2022 na kusomewa mashtaka yao na wakili wa Serikali Yusuph Aboud akisaidiana na Tumani Mafuru, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mery Mrio.

Akiwasomewa mashtaka yao, wakili Aboud amedai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na PI namba 9/2022.

Wakili Aboud amedai katika shitaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Oktoba 21, 2014 katika eneo la Magomeni Makanya Wilaya ya Kinondoni, walisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gramu 5309.57 zikiwa na thamani ya zaidi ya Sh265.47 milioni.

Shtaka la pili, siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina Cocaine zenye uzito wa gramu 894.28, zikiwa na thamani ya zaidi ya Sh62.59 milioni.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mrio amesema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiza kesi hiyo isipokuwa kwa kibali maalumu.

Upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mrio ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 21, 2022 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kabla ya leo, kufikishwa mahakamani hapo, washtakiwa hao walikuwa na kesi (Criminal Session namba 123/2016) ambayo ilikuwa katika hatua ya usikilizwaji Mahakama Kuu, lakini Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) aliifuta kesi hiyo na kisha kuwafungulia nyingine yenye mashtaka kama hayo.

Hata hivyo, huo ni utaratibu wa kawaida kwa upande wa mashtaka kufuta kesi na kuwafungulia nyingine iwapo watabaini kuna kasoro za kisheria katika kesi hiyo.


Mbali na Chonji, washtakiwa wengine ni Abdul Chumbi, Rehani Umande, Tanaka Mwakasagule na Maliki Maunda.