Chunya waadhimisha Muungano kwa kufanya usafi

Baadhi ya wananchi wa Halmshauri ya Wilaya ya Chunya wakifanya usafi eneo la Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Muungano wa Tanzania. Picha na Mary Mwaisenye

Muktasari:

Katibu tawala wa wilaya hiyo Anaklet Michombero amesema wao wameamua kuadhimisha kwa kufanya usafi kwa kushirikiana na wananchi katika hospitali lengo likiwa ni kutaka kuenzi Muungano huo.

Chunya. Wananchi wa Halmshauri ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wameadhimisha miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya usafi katika hospitali ya Wilaya ya Chunya, huku viongozi wakitumia maadhimisho hayo kusisitiza amani na kushiriki sense.

Akizungumzia maadhimisho hayo leo April 26, KatibuĀ  tawala wa wilaya hiyo Anaklet Michombero amesema wao wameamua kuadhimisha kwa kufanya usafi kwa kushirikiana na wananchi katika hospitaliĀ  lengo likiwa ni kutaka kuenzi Muungano huo.

Michombero pia amesisitiza kauli mbiu ya muungano isemayo, "Uwajibikaji na uongozi bora tushiriki sensa ya watu na makazi kwa maendeleo yetu," akiwataka wananchi kujiandaa kuhesabiwa ifikapo agosti 23 2022 ili kujenga uchumi imara.

Naye Mkurugenzi wa halmshauri, Tamimu Kambona ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi kwa kwa namna walivyo jitoa kushiriki usafi katika hospitali ya wilaya kwa kuhakikisha mazingira ya hospitali yanakuwa safi na salama.

Aidha katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Chunya Charles Jokery akizungumza baada ya kufanya usafi katika eneo la hospitali amesema moja ya mafanikio ya muungano huo pamoja na maendeleo ya miradi mbalimbali yanayo onekana.

Ambapo amesisitiza wananchi kudumisha amani na mshikamano uliopo ili nchi iendelee kuwa na amani.