CUF ilivyoibwaga ACT ubunge wa Eala

Baadhi ya wabunge wapya wa Bunge la Afika Mashariki (upande wa kulia) wakipongezwa na mawaziri bungeni baada ya kutangazwa washindi wakati wa uchaguzi uliofanyika Bungeni jijini Dodoma jana. Picha na Said Khamis 

Muktasari:

  • Ukiachana na matokeo ya kupiga kura za kuwapata wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), macho ya wengi yalikuwa kwenye mchuano wa nafasi ya kiti cha upinzani kilichokuwa kikiwania na wagombea watatu kutoka vyama vya CUF na ACT- Wazalendo.


Dar es Salaam. Ukiachana na matokeo ya kupiga kura za kuwapata wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), macho ya wengi yalikuwa kwenye mchuano wa nafasi ya kiti cha upinzani kilichokuwa kikiwania na wagombea watatu kutoka vyama vya CUF na ACT- Wazalendo.

ACT Wazalendo na CUF vilichuana baada ya Chadema kususia kikisema hakijabadili msimamo wa kutoyatambua matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Katika uchaguzi wa mwaka 2017, CUF na Chadema ndivyo vilivyoshiriki na viliwania nafasi tatu kati ya tisa, lakini mwaka huu nafasi ilikuwa moja kulingana na uwiano wa wabunge.

Katika mchakato wa jana, CUF ikiwa na wagombea wawili, ilichuana ACT-Wazalendo iliyokuwa na mgombea mmoja katika kuwania kundi la wapinzani. Mgombea wa CUF, Mashaka Ngole alimbwaga, Ado Shaibu ambaye ni Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo.

Matokeo ya uchagui huo yaliyotangazwa na Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi aliyesema Ngole alipata kura 234, Shaibu (78) na Jafari Mneke wa CUF alipata kura saba.

Mwihambi alisema katika kundi B linalojumuisha wagombea wa Zanzibar, kura 322 zilipigwa huku Dk Abdullah Hasnuu Makame alipata kura 305, Machano Ali Machano 291, Husna Abdu (4), Habib Mohamed Mnyaa (7) na Anderson Ndambo (2).

“Katika kundi A lililojumlisha wagombea wanawake jumla ya kura zilizopigwa ni 322, Angelah Kizigha amepata kura 322, Nadra Mohammed 310, Shogo Mulozi 322, Queen Lugembe tisa , Zainab Abdul moja. Kundi la Tanzania Bara jumla ya kura 322 zilipigwa huku tisa zikiharibika Ansar Kachwamba 300 na James Millya 312

“Dk Ng’waru Maghembe 311, Adui Kondo 10, Mohammed Ngulangwa tatu na Thomas Malima,” alisema Mwihambi wakati akitangaza matokeo hayo.

Katika mchakato huo, CCM iliwapeleka wagombea wanane, wakati ACT-Wazalendo wakimpeleka mmoja baada ya Pavu Abdallah kutokea Zanzibar kujiondoa dakika za mwisho. CUF kilipeleka wagombea 12 waliokwenda kushindanishwa katika makundi manne kwa mujibu wa utaratibu wa mchakato huo.

Maslahi ya Taifa kuyaweka mbele ndio kilikuwa mojawapo ya kipaumbele cha miongoni mwa wagombea hao 20 waliojinadi na kuomba kura kwa wabunge.

Kizigha aliyekuwa wa kwanza kujinadi alisema, “nina uwezo wa kutosha wa kusimama na kutetea masilahi ya Taifa katika Bunge la Eala. Nataka nikuhakikishe mheshimiwa Spika na wabunge humu nimejidhatiti na nina uwezo wa kulinda maslahi ya Taifa kama kipaumbele changu namba moja.

Aliyefuata ni Nadra aliwaomba wabunge akisema akipata nafasi hiyo kipaumbele chake kimojawapo ni kusimamia masilahi ya Taifa.

“Nitakuwa mstari wa mbele kuhamasisha amani na umoja miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya hii. Mheshimiwa Spika na wabunge kwa unyenyekevu naomba kura zenu,” alisema Nadra huku akishangiliwa kwa kupigiwa makofi na wabunge.