Daladala mbioni kuanza tiketi mtandao

Muktasari:

  • Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imesema inatarajia kuanzisha mfumo wa matumizi ya tiketi mtandao, utakaomfanya abiria kulipa nauli ya daladala kwa kadi.

Dar es Salaam. Katika siku za hivi karibuni, hautalazimika tena kutembea na nauli mkononi kwa ajili ya kupanda daladala, baada ya mpango wa Serikali kutumia tiketi mtandao katika usafiri huo.Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zinatarajia kuanzisha mfumo wa matumizi ya tiketi mtandao, utakaomfanya abiria kulipa nauli ya daladala kwa kadi.

Utekelezwaji wa hilo kwa mujibu wa Latra, utafikiwa baada ya kusimikwa mfumo utakaoingiliana na ule wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), ili kumruhusu abiria kufanya malipo ya nauli ya usafiri huo kwa kadi.Akizungumza na Mwananchi Digital kuhusu hilo, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri Ardhini wa Latra, Johansen Kahatano amesema hatua za mwanzo za ujenzi wa mifumo itakayounganishwa na BRT zimeshaanza.

"Tukikamilisha ujenzi wa mifumo, mifumo ya daladala na BRT itaoana ili kuruhusu abiria kutumia kadi katika aina zote za usafiri yaani wa BRT na daladala,” amesema.

Kulingana na Kahatano, hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi, kuboresha mifumo ya uendeshaji, kunusuru abiria kutozwa nauli isiyostahili, kukomesha wapiga debe, kuhamasisha malipo ya mtandao na kuiwezesha Serikali kukusanya mapato.

Baada ya kuanza kwa mfumo huo, Kahatano amesema wamiliki wa daladala watapokea fedha kulingana na safari zilizofanyika, tofauti na sasa ambapo dereva anawekewa kiwango cha fedha anachopaswa kuwasilisha kwa mmiliki.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kwa sasa wamiliki wa daladala wanahamasishwa kuunda makundi au kuanzisha kampuni ili kurahisisha malipo ya nauli kwa abiria.“Mfano daladala kutoka Tabata kupitia Chang’ombe kwenda Kivukoni, tunahitaji angalau mabasi 25 yawe katika makundi ili kutoa huduma,” amesema.

Hata hivyo, taarifa kuhusu kuanzishwa kwa mfumo huo si jambo jipya kwa kuwa  limeshawekwa hadi katika sheria ya mamlaka hiyo, kama inavyoelezwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Shifaya Lema.Amesema Latra imekuwa na matarajio ya kuanzisha mfumo huo kwa muda mrefu kwa masilahi ya kuwanufaisha wafanyabiashara ya usafiri wa daladala.

Hata Darcoboa amesema imekuwa ikitamani kuanza kwa mfumo huo ili wanufaike na biashara ya daladala, kwa kuwa utaratibu wa sasa dereva anaamua lini awasilishe na lini asiwasilishe fedha kwa mmiliki.“Iwapo mfumo wa tiketi mtandao utaanza, utatufaidisha wamiliki, madereva, makondakta na Serikali itapata mapato yake.

Jambo muhimu zaidi ni kwa Latra kuingia mikataba na kampuni sahihi zitakazokuwa na uaminifu katika ukusanyaji nauli,” amesema. Lema amesisitiza kwa kuitaka Latra kuanza kwa kuwajengea uelewa wamiliki wa daladala kabla ya utekelezwaji ili wasione kama jambo jipya.

"Hata zamani, baadhi ya wamiliki wa daladala hasa yale mabasi ya Eicher, walianzisha mfumo huo lakini kwa bahati mbaya hawakufanikiwa na hatujui kwanini. Tumeona baadhi ya mabasi ya mikoani bado yanaendelea kutoa tiketi za kawaida kwa abiria,” amesema.

Mmoja wa abiria, Juma James amesema tiketi mtandao zimeonekana kushindwa kutumika ipasavyo katika mabasi ya mikoani, hivyo si sawa kuanzishwa katika daladala.

"Latra inapaswa kuanza na kuimarisha tiketi mtandao katika mabasi yanayosafiri umbali mrefu na BRT kwa sasa, maana hayatumii kadi na mabasi mengi ya mikoani yanatoa tiketi za kawaida,” amesema.Amesisitiza si abiria wote wanaelewa kuhusu tiketi mtandao na namna zinavyofanya kazi.

"Ni muhimu kwa mamlaka kujenga uelewa kabla ya kufikiria kuanzisha mfumo huo. Namna ya uendeshaji, namna utakavyofanya kazi na jinsi wanafunzi watakavyoweza kuutumia bila kubughudhiwa na makondakta,” amesema.