Dar Group, Chato zachukuliwa na JKCI

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akizungumza na baadhi ya wagonjwa waliofika hospitali ya JKCI Dar Group leo kupata matibabu

Muktasari:

Miezi miwili baada ya Hospitali ya Dar Group kuchukuliwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Serikali imeagiza taasisi hiyo kwenda kuwekeza nguvu kubwa katika Hospitali ya Rufaa Chato itakayoanza kutoa matibabu ya kibingwa ya moyo.

Dar es Salaam. Serikali imeagiza Hospitali ya Dar Group iliyochukuliwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ijikite katika matibabu ya moyo ya watoto chini ya miaka 15, huku ikitoa maelekezo kwa taasisi hiyo kwenda kuwekeza katika Hospitali ya Chato.

Dar Group ambayo ilikuwa chini ya Wizara ya Fedha kwa kipindi kirefu, ilikabidhiwa kwa Wizara ya Afya mwishoni mwa mwaka jana.

Maagizo hayo yametolewa leo Jumamosi, Januari 14, 2023 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipotembelea hospitali hiyo kwa ajili ya ukaguzi kabla ya kuanza mradi wa upanuzi wa JKCI Dar Group utakaogharimu Sh5 bilioni.

“Upanuzi unaaanza JKCI Dar Group na ninawaagiza mkajikite zaidi katika matibabu ya moyo kwa watoto wa umri wa chini ya miaka 15.

“Sijasema msitoe matibabu kwa wagonjwa wengine wa moyo ila angalieni kipaumbele, huduma shirikishi mkaendelee nazo ila si kwa kipaumbele,” ameagiza.

Ameagiza pia vituo vya Dar Group Mbeya na Morogoro vifungwe na nguvu kubwa ielekezwe katika Hospitali ya Rufaa Chato.

“Serikali inataka Chato ijikite katika matibabu ya moyo Kanda ya Ziwa ili tuhudumie Watanzania wa kanda hiyo na tuwapate Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) itakua ni alama kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita,” amesema.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Peter Kisenge amesema miezi miwili tangu taasisi hiyo ikabidhiwe hospitali hiyo, kumekuwa uboreshaji wa huduma hali iliyoleta ongezeko la wagonjwa kutoka 300 kwa siku mpaka kufikia 400 mpaka 600.