Dar kinara ufaulu matokeo darasa la saba

Dar kinara ufaulu matokeo darasa la saba

Muktasari:

Katika mpangilio wa mikoa na halmashauri, manispaa na jiji kiufaulu, mkoa wa Dar es Salaam umeonyesha kuongoza kitaifa kwa asilimia 93.50 katika matokeo yake ikilinganishwa na mikoa mingine 31 ya Tanzania Bara na Visiwani.

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limesema mkoa wa Dar es Salaam umeonyesha kuongoza kitaifa kwa asilimia 93.50 katika matokeo yake ikilinganishwa na mikoa mingine 31 ya Tanzania Bara na Visiwani.

Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na idadi ya shule 671 na ulikuwa na watahiniwa 81,677 na waliofaulu kati ya daraja A mpaka C ni asilimia 93.50.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi, Novemba 21, 2020 na Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Charles Msonde wakati akitoa taarifa ya matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi uliofanyika Oktoba, mwaka huu.

“Shule hizi tumezipanga katika mpangilio wa mikoa na halmashauri, manispaa na jiji kiufaulu, katika mikoa iliyoongoza ni Dar es Salaam ulioshika nafasi ya kwanza, Arusha nafasi ya pili kwa kupata asilimia 92.42 na namba tatu ni Simiyu yenye asilimia 91.98,” amesema Dk Msonde.

Mkoa unaofuatia ni Katavi wenye asilimia 91.06 kiufaulu ukifuatiwa na Kilimanjaro (88.84) Iringa (88.56) Kagera (88.28) Morogoro (87.21) Pwani (86.99) na mkoa wa Mwanza uliofaulisha kwa asilimia 86.71.

Hata hivyo, Dk Msonde amesema mikoa mitatu iliyoongoza kwa ufaulu kwa miaka mitatu mfululizo ni Simiyu, Mara na Lindi na mikoa miwili iliyoshuka ufaulu ni Mtwara na Singida.