Dar yawaongezea siku 12 wamachinga kuondoka

Dar yawaongezea siku 12 wamachinga kuondoka

Muktasari:

  • Serikali ya mkoa wa Dar es Salaam imewaongezea wafanyabiashara ndogo ndogo (wamachinga) siku 12 kuanzia leo wahame katika maeneo yasiyo rasmi wanayofanyia biashara zao.

Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam imewaongezea siku 12 wafanyabiashara ndogo ndogo (wamachinga) kuanzia leo wahame katika maeneo yasiyo rasmi wanayofanyia biashara zao.

Awali Serikali ya mkoa huo iliagiza kuwa leo ndiyo iwe mwisho kwa wafanyabiashara hao kufanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi.

Uamuzi wa kuongeza siku hizo 12, umetolewa leo, Jumatatu Oktoba 18,2021 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wa Kariakoo kuhusiana na mpango wa kuwaondoa.

Makalla amesema ameamua kuwapa muda huo ili kila mmoja aweze kwenda katika eneo atakalokuwa amepangiwa na baada ya hapo hatataka kusikia kisingizio chochote.

"Nawapa muda mpaka Oktoba 30, baada ya hapo sitaki kusikia kisingizio chochote labda mtu aje na malalamiko kwamba kaenda kwenye maeneo yaliyotengwa kakosa nafasi," amesema Makalla.

Makalla ametaja maeneo ambayo wafanyabiashara hao wanatakiwa kuondoka kuwa ni kwa wale walio juu ya mifereji na mitaro,kwenye hifadhi za barabara  na mbele ya shule za Serikali au taasisi za Serikali.

Maeneo mengine wasiotakiwa kuwepo wafanyabiashara hao ni njia za waenda kwa miguu na wale waliopo mbele ya biashara za maduka ya watu.