Daraja lajengwa kuokoa wanawake, wanafunzi

Muonekano wa daraja jipya linalojengwa katika Mto Mwanzagamba Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu chini ya usimamizi wa Tarura kupitia Mpango wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

What you need to know:

Mto Mwanzagamba uliokuwa kikwazo kwa wanawake wa Kata ya Mwanyahina kwenda kupata huduma za afya ikiwemo kujifungua katika Hospital ya Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu umepatiwa ufumbuzi baada ya kujengewa daraja.

Meatu. Mto Mwanzagamba uliokuwa kikwazo kwa wanawake wa Kata ya Mwanyahina kwenda kupata huduma za afya ikiwemo kujifungua katika Hospital ya Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu umepatiwa ufumbuzi baada ya kujengewa daraja.

Wakizungumza leo Jumamosi Aprili 29, 2023 wakati wa ukaguzi wa njia zilizofunguliwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) msimu wa 2022/2023 wilayani humo, wakazi wa eneo hilo wamesema ilikuwa ni kazi ngumu kuvuka upande wa pili.

Wamesema hasa ikizingatiwa kuwa mto huo umekuwa ukifurika maji unayopokea kutoka sehemu mbalimbali hata kama eneo hilo hakuna mvua iliyonyesha.

Mkaazi wa Kijiji cha Buganza, Joseph Jagadi amesema wanawake wengi wamefia katika mto huo kwa kushindwa kuvuka wanapokwenda kutafuta huduma za uzazi katika Hospital ya Wilaya ya Meatu.

"Mfano  miezi miwili nyuma kuna mwanamke alifia hapa baada ya kushindwa kuvuka kutokana na mto kujaa hivyo ninaishukuru Serikali kwa kuamua kumaliza kilio cha muda mrefu cha wananchi," amesema Joseph

Mkazi wa Kiijiji cha Buganza, Minza maduhu amesema hakukuwa na utaratibu wowote wa kuvusha watu ambapo watoto wanaosoma upande wa pili wa mto walikuwa wanapata changamoto kuhudhuria masomo wakati wa mvua lakini pia mazao yaliuzwa kwa bei ya chini kwa sababu ya gharama kubwa za usafirishaji.

Mkunga wa kijijini hapo, Elizabeth Ndulu amesema hata watoa huduma za afya hospitalini waliifahamu changamoto ya mto huo iliyosababisha kinamama wengi wanaotoka upande wa pili wa mto kushindwa kujifungulia hospitalini.

Ujenzi wa daraja hilo umegharimu Sh70 milioni ikiwa ni miongoni mwa madaraja matatu yanayojengwa kwa gharama hiyo hiyo kupitia Mpango wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) na ajira za muda kwa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini.

Msanifu wa Ujenzi Ofisi ya Tarura wilayani humo, Maduhu Vicent amesema mradi huo uliibuliwa na wananchi na kufadhiliwa na Tasaf hivyo wao ni wasanifu pamoja na wasimamizi kuhakikisha ubora wa daraja hilo.

"Teknolojia ya kutumia mawe katika ujenzi wa daraja hili ni rahisi na inakidhi mahitaji ya wananchi hivyo tunatarajia ujenzi utakamilika ifikapo June, 2023 na daraja litaanza kutumika," amesema Maduhu