Dawa za mvuto wa mapenzi, nguvu za kiume zinavyotesa wanafunzi

Wauzaji wa dawa za asili wakiwa nje ya mlango wa kuingilia katika Shule ya Sekondari Viwandani iliyopo jijini Dodoma. Picha na Habel Chidawali

Dodoma. Biashara ya dawa za miti shamba na hasa zinazohusu mvuto wa mapenzi na nguvu za kiume, zinaweza kuwa janga kwa shule mbili za sekondari Dodoma na Viwandani jijini hapa.

Mwananchi lilifanya uchunguzi kwa siku kadhaa kwenye shule hizo na kugundua wafanyabiashara walioweka meza zao za dawa za miti shamba wakitazamana na mageti ya shule hizo, wateja wao wakubwa ni wanafunzi.

Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini wanafunzi wa kiume na kike ndio wanaokwenda kununua dawa za kumvuta mpenzi na nguvu za kiume kwa wafanyabiashara hao.

Dawa hizo zinauzwa na watu kwenye meza huku kukiwa na mabango madogo yanayobeba ujumbe wa kueleza faida ya dawa hizo.

Mabango hayo yanasomeka: “Dawa ya kuongeza uume, mvuto wa mapenzi, dawa za kukufanya uchelewe kufika kileleni (mkambaku) mundende’ na dawa ya kumfanya mpenzi kukurudia hata kama alikuwa amekuacha.”

Mbali na mabango hayo pia karatasi yenye orodha ya magonjwa yanayotibiwa na baadhi ya dawa hizo ambazo sehemu kubwa wauzaji wake ni jamii ya wafugaji.

Hata hivyo, baadhi ya wasichana waliohojiwa na gazeti hili, walidai wao hununua shanga kwa ajili ya kuvaa masuala ya dawa hawajihusishi nayo.

Shule hizo zipo katikati ya jiji la Dodoma karibu na soko la Sabasaba ambapo Viwandani ina wanafunzi mchanganyiko kwa kidato cha kwanza hadi cha nne wakati Sekondari ya Dodoma ina wanafunzi mchanganyiko wa kidato cha kwanza hadi cha nne, huku wa kidato cha tano na sita ni wasichana pekee.


Kinachofanyika

Katika uchunguzi huo mwandishi wa makala haya alishuhudia mara kadhaa wanafunzi wa kiume wakienda kuzungumza na wafanyabiashara hao kwa kunong’onezana na wao hutoa pesa na kupewa vitu vilivyofungwa kwenye karatasi.

Nembo walizoshonewa mabegani na aina ya sare zinawatambulisha kwa vidato vyao na shule wanazosoma kati ya hizo mbili, ingawa kwa idadi ndogo kuna wengine wanakuwa na sare zisizofanana na shule hizo ama ni vijana wa umri huo lakini hawana sare za shule.

Hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kinachotolewa hapo huwa ni dawa au vitu vingine, lakini mabadilishano ya fedha na karatasi zilizokunjwa yapo na yanafanyika.


Kauli ya wanafunzi

Mwanafunzi Yohana Charles (siyo jina lake) ambaye anasoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Viwandani, alikiri kutumia dawa hizo akisema huwa zinampa ‘vaibu’ wakati wa wa kujamiiana. “Mpenzi wangu ni mfanyakazi kwenye mgahawa mmoja uliopo eneo la Ipagala ambaye ni mwenyeji wa Mpwapwa anapenda mambo hayo na ana uwezo wa ziada. “Nisipotumia hizi dawa kuna hatari akaniacha akaenda kutafuta mtu mwingine, kwani anauweza na kuupenda sana huu mchezo. “Father (baba) umeniuliza kama natumia nilikataa, nimekujibu kwa heshima yako na kweli usitaje jina langu watanishughulikia, habari ya napata wapi fedha huko unakwenda kwingine, miaka 16 nisijue mapenzi si nitakuwa ‘bwabwa’, naweza kukuambia wananijua wenyewe mkali wao sema hizo dawa za kulevya kweli hata bangi mi ‘simaindi’ (hatumii),” anasema.

Anasema wanauziwa kuanzia Sh2,000 kwa kipimo kidogo huku akieleza watu wazima wanatumia dawa za mavumba na mizizi ya kuchemsha wakati rika lake wanatumia mavumba kwenye maji au soda.

Akizungumza kwa hofu, msichana anayesoma kidato cha nne Shule ya Sekondari Dodoma, anasema hajawahi kununua dawa za mvuto wa mapenzi lakini amekuwa akivaa shanga tangu akiwa kidato cha pili.

Anasema hajihusishi na suala la mapenzi kwani anajitambua, lakini kuvaa ushanga siyo jambo baya kwake kwa kuwa ni utamaduni wa kabila lake na hata mama yake anajua.

Hata hivyo, alikiri kuwa amewahi kushuhudia baadhi ya wasichana wenzake wakinunua dawa za aina ya mavumba ambazo zinakuwa na masharti ya kuchanganya na mafuta kisha wanajipaka, lakini hajui zinatibu kitu gani.


Walimu wataja sababu

Mmoja wa walimu katika shule hizo ambaye aliomba jina lake lisitajwe, anasema mambo hayo yapo kweli, lakini ni vigumu kuwadhibiti wanafunzi wao kwani mbali na kuuziwa dawa hizo, lakini kuna biashara ya dawa zinazotibu magonjwa ya binadamu na mara nyingi watoto husingizia hicho.

Mwalimu mwingine anasema kuwa mbinu inayotumiwa na wanafunzi kuwa wanaandika vikaratasi na kuwatupia wauzaji kuhusu dawa wanazozitaka nyakati za asubuhi, hivyo wakati wa mchana wanakuta wamefungashiwa.

Akizungumzia biashara hiyo, Fatuma Hamisi anayefanya kazi ya usafi barabara za eneo hilo anakiri kuwa mara nyingi ameshuhudia wanafunzi wakinunua dawa kwa wauzaji hao, ingawa hajui zinahusu nini na kwamba wanaonunua ni wavulana na wasichana wa vidato vya tatu na nne.

Fatuma ambaye mtoto wake amemaliza kidato cha nne Shule ya Sekondari ya Dodoma, anasema mbali na kuwaona watoto waliovalia sare, lakini siku za mapumziko ya juma baadhi ya watoto hufika na kununua dawa na shanga za kuvaa kiunoni wakiwa hawana sare na hiyo ndiyo nafasi yao kukaa na kuzungumza zaidi na wauzaji.

“Wananunua dawa za mapenzi kweli sijui, lakini kununua haaa! Siyo siri bwana wanakwenda mara nyingi na kibaya zaidi ni kwamba hapa hapa mlangoni kuna kituo kikubwa cha bajaji hivyo wanashuka na kuchukua na kuondoka,” anasema Fatuma ambaye kwa uzoefu wake katika maeneo hayo, wanafunzi wengi anawafahamu kwa sura hivyo hata wasipovaa sare za shule anawatambua.


Daktari

Mtaalamu wa magonjwa ya binadamu, Dk Beatrice Ndahani kutoka Kituo cha Afya Makole, anataja mambo matatu yanayochangia vijana wengi kuonekana kuwa na upungufu wa nguvu za kiume na kukimbilia kwa waganga.

“Dawa ni kutokuwa na msongo wa mawazo wakati wa tendo, waongeze mvuto au nguvu za kiume wakati mwingine inasababisha ulemavu wa mtu kwa maisha yote kwani tiba hazizingatii utalaamu,” anasema Dk Ndahani.


Mamlala ya jiji wazungumzia

Akizungumza na gazeti hili, mwanzoni mwa mwaka Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema wanashughulikia kuwaondoa wanaofanya biashara za kuuza dawa asili katika maeneo ya shule, kwani si mahali salama kwa vijana.

Mwishoni mwa wiki Meya wa Jiji, Profesa Davis Mwamfupe alisema tayari ameshaagiza idara inayohusika kuwaondoa wauzaji hao ili kuepuka vishawishi kwa watoto.