DC afunga mgodi wa dhahabu

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita. Said Nkumba

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita. Said Nkumba ameufunga na kupiga marufuku shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu katika mgodi wa Rush Namba Choo, uliopo kata ya Katente wilayani hapa kutokana na mgogoro.

Bukombe. Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita. Said Nkumba ameufunga na kupiga marufuku shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu katika mgodi wa Rush Namba Choo, uliopo kata ya Katente wilayani hapa kutokana na mgogoro.

Mgogoro huo ni kati ya wachimbaji na wakazi wa maeneo yanayouzunguka mgodi huo wakigombea maduara ambapo wakazi hao wanadai kuwa mgodi huo uko kwenye makazi ya watu.

Nkumba alisema Serikali imesitisha shughuli za uchimbaji kuanzia Aprili 6, 2021 baada ya kupokea malalamiko kwa muda mrefu ambayo pia walishirikisha ofisi ya madini iliyotoa ushauri wa kisheria.

Christina Benedicto ni mmoja wa wakazi wa eneo hilo aliyefurahishwa na uamuzi wa kufungwa kwa mgodi huo, akisema kero iliyowakabili imeondolewa hivyo wataishi kwa amani.

Alisema kero walizokuwa wakizipata ni visima vya maji kukauka na kelele za majenereta zinazowafanya wanafunzi washindwe kusoma usiku.

Naye Jacob Bandola alisema watoto wa kike wako hatarini kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa kutoka kwa wachimbaji wenye vishawishi lukuki.

Emmanuel Mihayo alisema uwepo wa mgodi huo kwenye makazi ya watu ulisababisha wanunue maji kwenye mikokoteni kwa Sh4,000 hadi Sh5,000 kwa siku.

Munge Magumba alisema kero nyingine ni kelele za magari yanayofanya kazi usiku kucha yakisomba miti ya matimba na kufanya watoto kushindwa kulala, pia wapangaji sita aliokuwa nao wamehama.

Mwenyekiti wa Rush ya mgodi wa Namba Choo Katente, Albert Charles alisema eneo hili lilianzishwa mwaka 1983 baada ya kuonekana dhahabu kwenye shimo ambalo lilikuwa linachimbwa na mkazi wa kijijini hapo kwa ajili ya choo.

Charles alisema mwaka jana, Serikali ilitoa kibali cha kuchimba dhahabu miaka miwili lakini sasa imeamua kuufunga mgodi.