DC Hai aagiza kusakwa kwa muuguzi aliyegoma kutoa huduma
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amiri Mkalipa
Muktasari:
- Mkuu wa wilaya ya Hai, Amir Mkalipa aliahidi kwenda hospitalini hapo kuzungumza na watumishi ili kufahamu ni kwanini wamekuwa wakitoa lugha chafu kwa wagonjwa pamoja na kutoa huduma zisizoridhisha.
Hai. Mkuu wa wilaya ya Hai, Amir Mkalipa amemwagiza mganga mkuu wa wilaya ya Hai (DMO) kumsaka muuguzi wa hospitali ya wilaya hiyo aliyegoma kumchoma mgonjwa sindano baada ya mgonjwa huyo kumkatalia kununua dawa zake alizotaka kumuuzia hospitalini hapo.
Mkalipa amesema baada ya mgonjwa huyo kuandikiwa dawa na daktari, muuguzi huyo alimtaka asinunue dawa hizo hospitalini hapo na badala yake ampe fedha ili amuuzie dawa zake, jambo ambalo mgonjwa huyo alilikataa.
DC Mkalipa amesema baada ya mgonjwa huyo kukataa na kwenda kutafuta dawa sehemu nyingine, aliporejea muuguzi huyo alikataa kumchoma sindano.
Mkuu huyo wa wilaya ameyaeleza hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekeleza wa ilani ya ya uchaguzi yaCCM katika mkutano mkuu wa halmashauri ya wilaya hiyo.
“Juzi alikuja mwananchi mmoja hapa ofisini kwangu, huyu mgonjwa aliandikiwa dawa na daktari, sasa nesi aliyekuwa akimhudumia akamwambia ‘usiende kununua hiyo dawa, mimi ninayo, leta fedha nikuchome”, yule mgonjwa akakataa, akaenda kununua ile dawa na aliporudi akampa hiyo dawa na kumwambia amchome, yule nesi akakataa kumchoma ile sindano,” amesema.
Ameongeza kuwa: “Huyu mgonjwa aliyekataliwa kuchomwa sindano akaja ofisini kwangu kuniletea malalamiko, nikaagiza apigiwe simu laini hakupatikana, sasa DMO nakuagiza umtafute huyo nesi tumjue halafu tutaongea.”
Kutokana na malalamiko ya hospitali hiyo kuwa mengi, aliahidi kwenda hospitalini hapo kuzungumza na watumishi ili kufahamu ni kwanini wamekuwa wakitoa lugha chafu kwa wagonjwa pamoja na kutoa huduma zisizoridhisha.
Hata hivyo, mganga mkuu wa wilaya hiyo ambaye alikuwepo katika mkutano huo, Itikija Msuya alimwahidi mkuu huyo wa wilaya kuwa atamfuatilia muuguzi huyo kwa hatua zaidi.