DC Hai asema hatavumilia uzembe, rushwa
Mkuu mpya wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Amiri Mkalipa alizungumza na watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Hai wakati alipowasili kwa mara ya kwanza katika ofisi za Wilaya hiyo. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Mkuu mpya wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Amiri Mkalipa amesema atafanya kazi kwa misingi ya utawala bora na wa kisheria, haki na uwajibikaji ni moja ya vipaumbele vyake vya msingi katika wilaya hiyo.
Hai. Mkuu mpya wa Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro, Amiri Mkalipa amesema hatavumilia uzembe, rushwa na namna yoyote ile ya ufisadi katika wilaya hiyo na kwamba kila mtumishi aliyepo katika wilaya hiyo anapaswa kufuata utawala bora.
Amesema kila mmoja anayo nafasi ya kuwajibika katika nafasi aliyoaminiwa na Serikali na kuhakikisha migogoro ambayo ipo kwenye maeneo ya wananchi inatatuliwa kwa wakati.
Ameyasema hayo leo Februari Mosi, 2023 wakati alipowasili katika ofisi za Wilaya hiyo na kuzungumza na watumishi wa idara mbalimbali za wilaya hiyo.
"Namshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kuniteua kuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, niwaombe watumishi wenzangu tushirikiane kuijenga Hai yetu, tuko hapa kwa ajili ya kumsaidia Rais wetu, lakini Kila mtu hapa amepewa nafasi yake ya kumsaidia.
"Kila mmoja akatimize wajibu wake, akaheshimu utawala bora na wa kisheria na mimi kama kiongozi mwenzenu tutakwenda pamoja kwenye suala la utawala wa kisheria, watu wawe huru kutoa maoni, kazi yetu sisi ni kuwasikilza na kuwahudumia wananchi," amesema.
Amesema msingi wa uongozi lazima uwe uongozi uliobeba utawala bora na kuwataka watendaji kutosemwa kwa mabaya.
“Kila tunachokifanya tufanye kwa maana ya utawala bora, na mwisho tutapimwa kwa utendaji wetu, na waliotupa dhamani watatupima kwa utendaji wetu," amesema.
Amesema hatamwingilia mtu yeyote katika utekelezaji wake wa majukumu katika Kutimiza wajibu, uhuru na haki ili wilaya hiyo iendelee kubaki salama.