DC Handeni akemea imani za kishirikina kwa wagonjwa wa macho.

Mkuu wa wilaya ya Handeni Siriel Mchembe akisalimiana na baadhi ya wagonjwa ambao tayari wamefanyiwa upasuaji wa macho hospitali ya wilaya Handeni leo Oktoba 16. Picha na Rajabu Athumani

Muktasari:

  • Jumla wa wagonjwa 400 wa Macho wamejitokeza kupatiwa huduma za magonjwa hospitali ya Wilaya Handeni ambapo zaidi ya 100 wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho.

Handeni. Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Siriel Mchembe amewataka wananchi wenye magonjwa ya macho kufika hospitali kupata tiba badala ya kusema ni magonjwa ya kishirikiana na kubaki nyumbani.

Akizungumza na wagonjwa kutoka Wilaya za Handeni na Kilindi wenye matatizo ya macho katika utoaji wa huduma wa siku tatu, DC Mchembe amesema wagonjwa hao wasihusishe ugonjwa huo na imani za kishirikina.

Amesema baadhi ya wazee kutoka maeneo mbalimbali walikuwa ni wagonjwa ila hawakufikiria kwenda hospitali kwa madai kwamba wamerogwa ila wametibiwa na kupona.

"Umefanyika upasuaji kwa wagonjwa wa macho zaidi ya 100 ndani ya siku tatu, wengi ni wazee na ukiuliza sababu kwa nini wamechelewa kuja hospitali wanaeleza ni kutokana imani za kishirikina," amesema Mchembe.

Mganga mkuu Halmashauri ya Mji Handeni, Feisal Said amesema wananchi 400 wenye matatizo ya macho wamejitokeza, ambapo zaidi ya 100 wamefanyiwa upasuaji na kuweza kuona vizuri.

Amesema kutokana na idadi ya wagonjwa wengi waliojitokeza kuongezeka upasuaji wao utaendelea hadi Jumapili Oktoba 17.

Aidha, Katibu wa CCM Wilaya ya Handeni, Salehe Kikweo amewashauri wagonjwa waliopata tiba, kuhakikisha wanazingatia mashariti waliowekewa ili kuweza kupona kabisa.

Mkazi wa wilaya ya Kilindi Mdachi Ramadhani ameomba tiba hizo zifikishwe wilayani humo, kwani kwenye eneo hilo kuna wagonjwa pia ambao uwezo wa kusafiri ni mdogo kwako.

Aidha Monica Daniel mkazi wa Handeni ameishukuru serikali kwa huduma hizo ambazo wamepata bure kwani imewsaidia kupunguza gharama hasa usafiri na malazi, kwani wengi wao hushindwa gharama husika.

Matibabu hayo yalitolewa kwa siku tatu kuanzia juzi Oktoba 14 mpaka jumapili tarehe 17 kwa wagonjwa kupata tiba mbalimbali za macho zilizodhaminiwa na taasisi ya Mobile Eyes Foundation.