DC Jokate awaomba wadau kuchangia maendeleo ya elimu

Muktasari:

  • DC Jokate amewaomba wadau wa elimu nchini kusaidia jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha sekta ya elimu hapa nchini.

Dar es Salaam. Mkuu wa wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo amewaomba wadau wa elimu nchini kusaidia jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha sekta ya elimu hapa nchini.


Ameyasema hayo jana Oktoba 19 wakati akipokea msaada wa rangi za Coral Paints zenye thamani ya Sh15 milioni kwa ajili ya ukarabati wa shule ya msingi ya Kizinga, iliyopo Mbagala Kizuiani jijini Dar es Salaam.


DC Mwegelo amesema serikali imeweka kipaumbele uboreshwaji wa elimu kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa 15,000 nchi nzima na utengenezaji wa madawati.


Pia ameipongeza kampuni ya Insignia Limited inayozalisha rangi hizo kwa msaada huo wenye lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia shuleni hapo.


“Mmefanya jambo jema sana katika kuunga mkoni jitihada za Raisi Samia Sululhu Hassan za kuhakikisha wanafunzi wote wanasoma katika mazingira bora bila changamoto yoyote,” amesema Jokate.


Awali, mkuu wa shule hiyo, John Kaula alisema shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za uchakavu wa majengo, hivyo msaada huo utaufanya shule hiyo ipendeze zaidi na kutoa ari kwa wanafunzi wake ya kujifunza zaidi.


Naye Constantia Emmanuel, Afisa Elimu, Vifaa na Takwimu wa wilaya ya Temeke ameishukuru kampuni hiyo kwa kujibu maombi yao ya uhitaji wa ukarabati wa shule hiyo.


“Tulivyowafuata na kuwapa maombi yetu hamkusita na kuamua kutuunga mkono katika kuboresha sekta ya elimu hapa nchini,” alisema.


Baada ya kupokea msaada huo katika hafla fupi iliyohudhuriwa na wanafunzi wa shule hiyo, DC Jokate alitoa maagizo kwa kamati ya shule hiyo kusimamia vema msaada huo na kuanza ukarabati wakati wa likizo ya Desemba wanafunzi wakiwa majumbani na kuanza mwaka mpya na muonekano mpya wa shule yao.


Jokate alikabidhiwa msaada huo na Adam Kefa, mkuu wa kitengo cha Masoko wa kampuni hiyo ambaye amesema wamefanya hivyo katika kumuunga mkono Rais Samia kwa kuboresha mazingira ya shule hiyo wakati serikali pia ikitekeleza mahitaji mengine kama vile ujenzi wa madawati.


Mmoja wa wanafunzi hao, Sudi Hamidu anayesoma darasa la sita, kwa niaba ya wanafunzi wenzake, ameishukuru kampuni hiyo na kusema shule yao sasa itakuwa na muonekano mzuri zaidi wenye kuvutia.