DC Masala: Hatujafungia baa, tumezuia kelele za muziki

New Content Item (1)
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hasan Masala akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza. Picha na Saada Amir

What you need to know:

Baa zinazobainika kukiuka sheria ya mazingira kwa kupiga muziki kwa sauti ya juu kinyume cha sheria huchukuliwa hatua mbalimbali ikiwemo ama kuagizwa kusitisha kupiga muziki kwa sauti ya juu au kutozwa faini kati ya Sh2 milioni hadi Sh10 milioni kulingana na makosa.

Mwanza. Uongozi wa Serikali Mkoa wa Mwanza umekanusha madai ya kusitisha huduma katika baa 31 za mkoa huo, badala yake, kilichozuiwa ni tabia ya baadhi ya wamiliki na wafanyakazi wa baa kupiga muziki kwa sauti ya juu zinazoathiri jamii jirani.

Akizungumza na waandishi wa habari Mei 22, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hasan Masala amesema Serikali kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imechukua hatua hiyo kulinda afya ya wananchi kutokana na kelele za muziki unaopigwa kwa sauti kubwa kwenye baa na maeneo mengine ya burudani.

Masala aliyezungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makala, amesema Serikali imechukua hatua hiyo baada ya baadhi ya wamiliki kushindwa kutekeleza maelekezo kuhusu kiwango cha sauti za muziki kinachokubalika kisheria.

Amesema katika oparesheni ya kudhibiti kelele mitaani, NEMC ilifanya ukaguzi katika baa na maeneo ya burudani 50 ambapo baa 31 zilibainika kuzalisha kelele zinazopitiliza viwango vya kisheria.

Kutokana ukaguzi huo, Masala amesema baa zilizobainika kukiuka sheria zilichukuliwa hatua mbalimbali ikiwemo kuagizwa kusitisha kupiga muziki kwa sauti ya juu, kulipishwa faini kati ya Sh2 milioni hadi Sh10 milioni kulingana na makosa huku wanaorudia makosa baada ya kutozwa kiwango cha chini cha Sh2 milioni wakitozwa faini ya Sh5 milioni.

“Umma ufahamu kuwa ni muziki unaopigwa kwa sauti ya juu pekee ndiyo umezuiliwa; Serikali haijazuia shuguli nyingine ikiwemo ya kuuza vyakula na vinywaji,’’ amesema Masala

Ufafanuzi huo umekuja huku kukiwa na taarifa zinazozunguka kupitia mitandao ya kijamii kuwa wamiliki wa baa mkoani Mwanza wanakusudia kugoma kupinga uamuzi wa NEMC kufunga shughuli zao.

Masala amewashauri wamiliki wa baa kufunga vifaa vya kupimia sauti ili kujidhibiti wenyewe kuondoa misuguano na mamlaka za Serikali.

Jumanne Shao, mkazi wa jiji la Mwanza ameipongeza Serikali kwa kuzuia kelele za muziki unaopigwa kwa sauti ya juu katikati ya makazi ya watu huku akiomba udhibiti huo kuelekezwa pia kwenye baadhi ya nyumba za ibada zinazofanya maombi ya mikesho kupitia vipaza sauti vinavyofunguliwa kwa sauti ya juu.

‘’Kila mtu anayo haki ya kuabudu; lakini haki hiyo haistahili kuwakwaza wengine. Kitendo cha kufanya ibada za mikesha kwa kutumia vipaza sauti katikati ya makazi ni kero kubwa jijini Mwanza katika siku za hivi karibuni,’’ amesema Shao

Hoja hiyo imeungwa mkono na Isaac John, mkazi wa mtaa wa Nyabulogoya jijini Mwanza akishauri utekelezaji wa sheria ya mipango miji inayoelekeza maeneo ya huduma zote za kijamii kuanzia makazi na nyumba za ibada.