DC Mtanda ‘awakwepa’ madiwani

Tuesday December 15 2020
mtanda pic

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda.

Sumbawanga. Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda amesema hatokubali kutumika kuwashawishi madiwani wa halmashauri hiyo kukubali kufanya vikao bila kulipwa posho zao.

Amebainisha kuwa madiwani hao wana jukumu la kuhakikisha wanashirikiana vyema na watendaji wa halmashauri yao kubuni vyanzo vipya vya mapato ya ndani ili fedha zitakazopatikana zisaidie kutekeleza miradi ya maendeleo na kulipa posho zao.

Ameeleza hayo leo Jumanne Desemba 15, 2020 katika kikao cha baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Nkasi.

Amesema madiwani wanaposikia halmashauri haina fedha za kuwalipa wanagoma kufanya vikao kwa mujibu wa taratibu.

"Madiwani niwasihi simamieni ukusanyaji wa mapato ya halmashauri ili masuala ya maendeleo yafanyike na nyie msiwe mnalialia kuhusu posho zenu za vikao..., mkumbuke kuna wengine hadi wanaondoka hawajalipwa baadhi ya madeni yao," amesema Mtanda.

Katika kikao hicho Pancras Maliyatabu alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo na makamu wake, Wensilaus Kapita.

Advertisement

________________________________________________________________

Na Mussa Mwangoka, Mwananchi [email protected]

Advertisement