DC Musoma aagiza wahujumu miundombinu ya maji wakamatwe

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule amesema vitendo vya uhujumu wa miundombinu ya maji vimekithiri katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini na hivyo kuwataka wenyeviti na kamati za maji kulinda miundombinu hizo.


Musoma. Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule amesema vitendo vya uhujumu wa miundombinu ya maji vimekithiri katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini na hivyo kuwataka wenyeviti na kamati za maji kulinda miundombinu hizo.

Dk Haule ametoa kauli hiyo katika mji wa Mugango wilayani Musoma leo Juni 23, 2022 katika kikao cha utoaji wa taarifa juu ya utekelezaji wa miradi ya maji katika halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Amesema kuwa kutokana na kukitihiri kwa vitendo hivyo walengwa wa miradi ya maji wamekuwa  wakikosa huduma ya maji hivyo kuagiza kusakwa na kukamatwa kwa watuhumiwa wote wanaojihusisha na uhujumu wa miundombinu hiyo.

Amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2021/22 Serikali ilitoa zaidi ya Sh3 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi sita ya maji na kwamba endapo vitendo hivyo vitaendelea kuwepo maelego ya serikali ya kuwapatia wananchi maji safi na salama hayatafikiwa.

"Mwaka ujao wa fedha tunatarajia kupokea Sh4 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi mingine tena ya maji sasa kama hizi changamoto zitaendelea ni dhahiri kuwa hatutafikia malengo," amesema.

Awali, akitoa taarifa juu ya upatikanaji wa maji katika halmashauri hiyo, mhandisi kutoka ofisi ya Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa), Innocent Edward alisema kuwa ofisi yake imeweza kusambaza majisafi na salama kwa asilimia 66.7 kwa wakazi zaidi ya 276,000 katika eneo hilo.

Kuhusu hali ya visima, Edward amesema kuwa visima 31 kati ya 71 vilivyochimbwa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika halmashauri hiyo havitoi maji huku sababu kuu ikiwa ni hujuma ya miundombinu yake.

"Asilimia 32 ya visima visivyofanyakazi vimehujumiwa, baadhi ya visima havifanyi kazi baada ya watu kuvamia na kuiba kila kitu mfano visima viwili kati ya vitatu katika Kijiji cha Kabegi havina kila kitu baada ya vifaa vyote kuibiwa," amesema.

Baadhi ya washiriki wa kikao hicho wamedai kuwa hali hiyo ya uhujumu wa miundombinu inatokana na Jeshi la Polisi kutokuwachukulia hatua watuhumiwa ambao wamekuwa wakifikishwa polisi kwa tuhuma za kuharibu miundombinu hiyo.


" Kuna mtu tulimkamata kwa kuharibu miundombinu lakini tulipomfikisha polisi mtendaji pamoja na mgambo waligeuziwa kibao na kuweka ndani ,jeshi la polisi linashirikiana na wahalifu  ndio maana vitendo hivyo vinaendelea kuwepo," amesema Majura Majura wa Kijiji cha Kusenyi.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Musoma ( OCD),Jumanne Mkwama amesema kuwa ili mtuhumiwa yeyote aweze kufikishwa mahakamani ni lazima upatikane ushahidi wa uhakika dhidi ya tuhuma zake na hivyo kuwataka wenyeviti wa vijiji kutoa ushirikiano pale wanapomfikisha mtuhumiwa yeyote polisi.

" Wengi mmelalamika hapa leo lakini tatizo lipo kwenu sisi hatuwezi kufanya lolote kama hakuna ushahidi, pia mnatakiwa kujua kuwa dhamana ni haki ya mtuhumiwa kwa hiyo mkimuona mtuhumiwa kaachiwa kwa dhamana msifikiri ni rushwa bali ni kwa mujibu wa sheria," amesema