DC Rombo apewa rungu kushughulikia wakandarasi
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Cyprian Luhemeja
Moshi. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Cyprian Luhemeja ampa rungu Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Kanali Hamis Maiga kuwabana na kuwakamata wakandarasi watakaochezea miradi ya maji wilayani humo.
Luhemeja amesema tayari serikali imetoa fedha nyingi kuhakikisha miradi ya maji wilayani humo inatekelezwa ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika wilaya hiyo.
Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua mradi wa maji wa Njoro 11 ambao utahudumia Tarafa tatu za Tarakea, Usseri na Mashati wilayani humo, Luhemeja alimtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi huo utakaogharimu zaidi ya Sh3 bilioni kuhakikisha unakamilika mwezi Juni mwaka huu.
"Serikali imeshatoa Sh732 milioni kumlipa Mkandarasi, nitumie nafasi hii kumwelekeza mkandarasi kwamba aliahidi mwezi juni kazi inakamilika na ikamilike kweli na DC huyu mtu ni saizi yako asipokamilisha mweke ndani maana wakandarasi wanastori nyingi sana, maana kwenye malipo tumeshajitahidi na malipo yake yanakuja,"alisema Luhemeja
Aliongeza; "Rombo wana changamoto ya vyanzo vya maji na Waziri wa maji alitoa maelekezo na nimekuja kukagua maendeleo ya maelekezo yake, na ameelekeza tutafute vyyanzo vingine vya maji na nashukuru watu wa Bonde la Pangani wamefanya utafiti mkubwa na wametambua sehemu saba za kuchimba kupata maji,"
Aidha, Luhemeja alisema lengo la serikali ni kuhakikisha ikifikapo 2025 vijiji vipate maji kwa asilimia 85 na mjini kwa asilimia 95 kwa mkoa wa Kilimanjaro.
"Rombo ndio kidogo imeshuka, wilaya ya Moshi tupo vizuri, Hai, na Siha hali sio mbaya sana kwa hiyo niwahakikishie Wizara ya maji tuko 'serious' na hii changamoto ni suala tu la muda na itaenda kukamilika,"
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Rombo (Rombowasa), Martin Kinabo alisema katika wilaya hiyo ipo miradi ya maji inayotekelezwa kwa Sh8 bilioni.
"Sasahivi kuna miradi ya takribani ya Sh8 bilioni ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, Ruwasa wanasiamamia miradi ya Sh6.4 bilioni na Mamlaka ya maji Rombo inasiamamia mradi wa Sh1.5 bilioni, tunaishukuru sana serikali yetu kupitia Wizara ya maji,"
"Mwaka jana serikali ilitusaidia sana, wizara ya maji ilitoa fedha Sh600 milioni ambapo tulinunua mita pamoja na vitu vingine na tuliweza kuwaunganishia wateja wetu, tulikuwa na wateja zaidi ya 5000 wakati kampuni ya Kiliwater inakabidhi Mamlaka lakini kwasasahivi na kwa namna tulivyosaidiwa serikali tumeweza kuwafungia wateja wote mita za maji," alisema Kinabo