DC Sophia alivyovuka vikwazo vya kazi, familia kupata PhD

Tangu akiwa mtoto siasa ilikuwa ndani ya damu yake, lakini kipaumbele chake kilikuwa kwenye elimu. Hilo lilimfanya awe miongoni mwa wanafunzi vinara darasani katika ngazi zote za elimu alizopitia kuanzia Shule ya Msingi Ngarenaro, Sekondari Ashira na Tambaza alikohitimu kidato cha sita na kupata ufaulu uliompa nafasi ya kusoma Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Miaka mitatu aliyosoma kwenye chuo hicho, bado aliendelea kuonyesha shauku yake kwenye elimu na kuwa miongoni mwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi na kutakiwa kubaki chuoni hapo kwa ajili ya kufundisha. Hata hivyo, hakuitumia nafasi hiyo baada ya kuzidiwa nguvu na upepo wa siasa.

Huyu ni Sophia Mfaume Kizigo (30), mkuu wa wilaya ya Mpwapwa ambaye hivi karibuni ametunukiwa shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuingia kwenye rekodi ya Watanzania wachache waliofikia ngazi hiyo ya elimu wakiwa na umri mdogo.

Binti huyu amedhihirisha kwa vitendo shauku yake katika kutafuta elimu, kwani licha ya majukumu makubwa aliyonayo katika kuhudumia wananchi kama kiongozi, bado ameweza kuendelea kuitafuta elimu na hatimaye kutunukiwa shahada ya uzamivu ndani ya miaka mitatu aliyoanza kusoma.

Mwananchi imefanya mahojiano maalumu na mkuu huyo wa wilaya ambaye amekiri haikuwa rahisi, lakini amefanikiwa kwa kuwa aliweka nia na jitihada na alihakikisha anatimiza majukumu yote yaliyo mbele yake.

“Siwezi kusema kwamba ilikuwa rahisi nitadanganya, nidhamu ya muda ndiyo kila kitu. Nilijitahidi kadiri ya uwezo wangu kuhakikisha lengo langu la kufanya PhD linafanikiwa bila kuathiri utendaji wangu kama mkuu wa wilaya na nashukuru Mungu nimefanikisha hilo ndani ya muda mfupi.

“Imenichukua miaka mitatu kuanzia niliposajili hadi kufanya utafiti na kuhitimu, naweza kusema ni muda mfupi kwa sababu wapo ambao inawachukua miaka sita hadi tisa. Kwa kuwa nilidhamiria kulifanya hili, basi nikajitahidi iwe ndani ya muda mfupi,” anasema Sophia.

Unaweza kujiuliza aliwezaje kujigawa hadi kufanikisha yote hayo? Mwenyewe anaeleza kuwa watu wanaozunguka wana mchango mkubwa katika hatua hiyo ya mafanikio.

“Nikianzia kazini watumishi wenzangu walielewa kwamba mkuu wa wilaya anasoma, hivyo walinisaidia katika kutunza muda. Pili mimi si mtu wa vikao vya muda mrefu wala kupoteza muda bila sababu ya msingi. Nikisema kikao ni saa tatu, basi itakapofika muda huo tutaanza na tumaliza kwa muda tuliopanga, iko hivyo hata kwenye maisha yangu nje ya kazi,” anaeleza.

Mbali na wafanyakazi wenzake, Sophia anasema familia yake imekuwa na msaada mkubwa na imechangia kumwezesha kutimiza azma yake ya kusoma.

“Wakati nimejisajili kwa ajili ya PhD nilikuwa mjamzito na Mungu akanijalia watoto pacha, sasa vuta picha malezi ya hao watoto, mimi pia ni mke, hivyo nina jukumu la familia, kazi ya ukuu wa wilaya na shule, lakini familia yangu haikuniacha, ilinisaidia kila nilipohitaji msaada.

“Kuna wakati mama yangu alikuwa ananisaidia kuwahudumia watoto ili nipate muda wa kusoma na kufanya majukumu mengine. Katika kipindi chote cha miaka mitatu nilikuwa najitahidi kwa siku lazima nipate saa mbili za kusoma na kuandika maana kwenye PhD ni kuandika zaidi,” anasema.

Mbali na hizo saa mbili anazotenga kwa ajili ya kusoma, Sophia amejitengenezea ratiba inayompa mwongozo wa kutimiza majukumu yake ya kila siku na kupata muda wa kupumzika kutokana kile anachoamini ili mtu aweze kufanya mambo kwa ufanisi ni lazima apate wasaa wa kupumzika.

“Hata ikitokea tunakwenda kwenye ziara, ni lazima nihakikishe saa tisa na nusu tumerudi ofisini, nafanya hivi si tu kwa ajili yangu bali hata kwa watumishi wenzangu, huwa najitahidi kila kitu kifanyike ndani ya muda wa kazi. Kwa utaratibu huo tunapata muda wa kurudi nyumbani mapema na kushiriki kwenye majukumu ya familia.

“Nikiwa mama najitahidi pia nipate muda wa kuwa na watoto, nafanya shughuli zangu za nyumbani kama nilivyosema mimi ni mke, hivyo kuna wakati lazima nipike kwa ajili ya familia yangu, kuwa mkuu wa wilaya hakunifanyi niachane na majukumu hayo,” anaeleza.

Marafiki pia wana mchango katika hatua aliyofikia Sophia kwa kuwa walitambua uwezo wake na walikuwa wakimtia moyo kwenye kila hatua ya elimu aliyokuwa akipiga.

“Marafiki zangu nilionao sasa ni wale niliokuwa nao tangu nikiwa sekondari, hivyo wananifahamu vizuri na mara zote wamekuwa wakinitia moyo.

“Nakumbuka nilivyomaliza shahada ya kwanza nilikaa mwaka mzima kabla ya kufanya masters, walikuwa wakinisukuma kuendelea kwa kuwa wanajua napenda kusoma. Leo nilivyofikia kupata PhD wamefurahi kwamba kati yao kuna mwenye shahada ya uzamivu,” anaeleza.
 

Shahada ya uzamivu inamuongezea nini kwenye utendaji?

Sophia anaeleza safari yake ya kuitafuta PhD imemfunza uvumilivu, utulivu katika kufanya uamuzi, ushirikiano na watu na udadisi kabla ya kuamua cha kufanya.

“Wakati nafanya utafiti, kuna vitu nilikuwa nafikiri hivi halafu majibu yamekuja tofauti, kwa hiyo sasa hivi siwezi kuamua kufanya kitu bila kukichambua na kuangalia kina tija gani. Pia imeniongezea ujuzi na maarifa katika eneo la mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu.

“Nilifanya utafiti Namtumbo kuhusu sababu za misitu ya jamii kuendelea kuharibika, nimepata majibu ya watu wanavyofikiria, naamini utafiti huu utasaidia watu kujua kwa undani. Utafiti wangu umechapishwa kwenye journal ya kimataifa na nimeuweka katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza kuwezesha kila anayehitaji kusoma afanye hivyo kwa lugha atakayoimudu,” anasema.
 

Historia yake katika siasa

Sophia ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto watano, alizaliwa mwaka 1993 na alianza kujitosa kwenye medani za siasa tangu akiwa mwanafunzi wa darasa la tatu ambako alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chipukizi wa Taifa, nafasi iliyompa fursa ya kuwa mjumbe wa baraza kuu la vijana Taifa na mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa.

Akiwa na miaka 19, aligombea na kufanikiwa kuchaguliwa kuwa mjumbe wa halmashauri kuu kupitia vijana, ikiwa ni muda mfupi baada ya kuhitimu kidato cha sita.

Hii ina maana kwamba wakati wote anasoma shahada ya kwanza alikuwa tayari kwenye ulingo wa siasa, lakini halikumfanya apoteze uelekeo kwenye masomo, hali iliyosababisha awe miongoni mwa waliotakiwa kubaki kufundisha chuoni hapo kutokana na kiwango kikubwa cha ufaulu.

Hata hivyo, Sophia hakubaki chuoni kwa kuwa mwaka huo aligombea ubunge kupitia vijana na akawa miongoni mwa vijana sita waliotakiwa kuwakilisha kundi hilo bungeni, lakini kutokana na kura za mgombea urais kutofikia kiwango kinachotakiwa, idadi hiyo ilipunguzwa hivyo hakupata nafasi hiyo.

Kabla hajamaliza kipindi cha pili cha ujumbe wake wa NEC, Rais wa Awamu ya Tano, hayati John Magufuli akamteua kwenye utumishi wa umma kama Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma akiwa na miaka 24.

Licha ya kuwa alishaanza kujihusisha na masuala ya siasa, kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya si jambo alilowahi kulifikiria, kwani akili yake ilikuwa ni kwenye kugombea ubunge ambao tayari alishafanya jaribio la awali.

Taarifa ya kuteuliwa kwake aliipata akiwa kwenye mizunguko yake baada kutoka chuoni Mzumbe alikokuwa anasoma shahada ya uzamili.

“Nakumbuka siku hiyo nilikuwa natoka zangu chuo nikapitia Kariakoo kuna vitu nilienda kununua. Unafahamu mazingira ya Kariakoo ni vigumu kuangalia simu kila wakati, hivyo ilikuwa kwenye mkoba. Nikiwa dukani kuna vitu niliagiziwa na mtu, sasa nikatoa simu nimpigie ndipo nikakuta nimepigiwa simu nyingi.

“Ile hali ilinishtua nilipoziangalia namba zote zilizonipigia nikaona nianze kumpigia baba, yeye ndiye aliyenipa taarifa za kuteuliwa kwangu, kiukweli nilishtuka hadi nikadondosha simu pale dukani. Nilimshukuru Mungu kwa heshima aliyonipitia, sikufikiria kama ningepata dhamana hiyo ya kumwakilisha Rais,” anasema Sophia.