DC Ubungo ataka utaratibu kwa wafanyabiashara stendi ya Magufuli

DC Ubungo ataka utaratibu kwa wafanyabiashara stendi ya Magufuli

Muktasari:

  • Siku chache baada ya kituo cha mabasi cha Magufuli kuzinduliwa rasmi, Mkuu wa wilaya ya Ubungo amemtaka mkurugenzi wa halmashauri ya Ubungo kutoa utaratibu ambao utawawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika kituo hicho.

Dar es Salaam. Mkuu wa wilaya ya Ubungo, Kisare Makori ametoa maelekezo kwa mkurugenzi wa wilaya hiyo akimtaka kutoa utaratibu rafiki kuanzia kesho utakaowawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa amani katika stendi mpya ya Magufuli iliyopo Mbezi Luis.
Makori ameyasema hayo leo Februari 28 wakati akizungumza na Mwananchi kuhusu kero na malalamiko yanayotolewa na wafanyabiashara wa kituo hicho ambao wanadai kuzuiwa kufanya shughuli zao licha ya Rais Magufuli wakati anazindua kituo hicho Februari 24 kuwaruhusu waendelee na shughuli zao.
Amesema baada ya kuzinduliwa kwa kituo hicho cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani, waliomba muda wa kutengeneza mfumo mzuri utakaowawezesha wafanyabiashara hao kuendelea na shughuli zao.
“Sio kwamba tuliwafukuza, baada ya Rais kutoa tamko sisi kama viongozi wa chini tunapaswa kulitekeleza na tuliomba muda kwao watupe muda wa kutengeneza utaratibu ambao utatolewa kuanzia kesho na mkurugenzi utakao utakaomwezesha kila mmoja wao kupata sehemu na kufanya shughuli zake kwa utaratibu.
“Tulikuja na mpango huo kwa lengo la kuwarahisishia wenyewe kwa sababu tulipata malalamiko kwamba kuna madalali wanachukua maeneo makubwa na kuwakatia wafanyabiashara kwa bei kubwa,” amesema Makori.
Kiongozi huyo amebainisha kwamba hawana matatizo na wafanyabiashara hao,isipokuwa wanatengeneza mfumo utakao warahisishia kazi zao.
“Tunakuja na utaratibu mzuri kwanza vijana wa bodaboda, bajaji na mama lishe tunawajengea mazingira yatakayowavutia hata wateja wao,” alisema.
Makundi matatu ya wafanyabiashara wanaolalamika ni wale waliotoka maeneo ya Mbezi baada ya upanuzi wa barabara, watu waliotoka stendi ya mabasi ya Ubungo na watu waliotoka sehemu mbalimbali za mji.