Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ded asimulia mfumo wa ununuzi ulivyompatia tuzo ya Sh10 milioni

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kwimba, Happiness Msanga akipokea Sh10 milioni kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa Jijini Dodoma. Picha na maktaba

Muktasari:

Tuzo hiyo alipewa Februari, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa Jijini Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo kwa halmashauri iliyoibuka kinara nchini katika matumizi ya Mfumo wa Taifa wa Manunuzi wa Kielektroniki (NeST).

Mwanza. Wakati baadhi ya watumishi wa umma wakidaiwa kukwepa matumizi ya mfumo wa ununuzi wa umma wa kielektroniki (NeST), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Happiness Msanga ameelezea namna mfumo huo ulivyompatia Sh10 milioni kama motisha kwa kufanya vizuri kati ya halmashauri zote nchini.

Baadhi ya sababu zilizoifanya Serikali kuzitaka taasisi zake kutumia mfumo huo ulioanza Oktoba, 2023 ni kudhibiti upotevu wa fedha za umma, rushwa, pamoja na mchakato wa ununuzi kuchukua muda mrefu.

Hata hivyo, baadhi ya wakuu wa idara wanadaiwa kuukwepa sababu zikitajwa ni uelewa mdogo unaosababisha kuwa na mitazamo hasi, huku halmashauri nyingine zikidai hazikuwa na mapato ya kulipia gharama ya Sh1.5 milioni ya kupandisha mpango huo.

Akisimulia leo Mei 21, 2024 wakati wa mafunzo ya kuwaongezea ujuzi wa matumizi ya mfumo huo wakuu wa taasisi, wajumbe wa bodi za zabuni, vitengo vya usimamizi wa ununuzi, idara tumizi, wakaguzi wa ndani, maofisa sheria na wataalamu wa mifumo wa Kanda ya Ziwa, Msanga amesema halmashauri yake ilipokea tuzo ya Sh10 milioni Februari 2024, iliyotolewa na Mchengerwa Jijini Dodoma.

Amesema alihakikisha idara zilizopo chini yake zinatumia mfumo huo hadi ilipofika Februari 2024, Serikali ilipokuwa inafanya tathmini ya matumizi halmashauri hiyo iliibuka kidedea kati ya taasisi zote za Serikali.

“Kwa hiyo, baada ya hilo, waziri alinipa tuzo na pongezi kwa usimamizi mzuri wa mfumo. Kwa mfano, halmashauri ya Kwimba ipo vijijini lakini tumeongoza, ina maana kuna vitu vingine ni mwenyewe kiongozi unavyojiongeza, labda radi zimepiga mitandao imezingua lakini kuna muda radi zitaacha tu, lakini mfumo huu ni rafiki maana unatumia hata mtandao wa simu kikubwa ni kuwa na team work (ushirikiano kazini), kazi zinaendelea,”ameongeza.

Faida za mfumo

Amesema pamoja na kupata tuzo hiyo, mfumo huo umesaidia kuondoa malalamiko ikiwemo ya upendeleo kwa wazabuni lakini pia unaendana na bei ya soko.

“Mzabuni akiomba, mfumo wenyewe ndio unachagua nani kashinda, kwa hiyo automatically (moja kwa moja) kunakuwa na ushindani wa usawa. Ni mfumo bora kwa sababu wanaoshindana hawajulikani, kwa hiyo bei yako ndiyo itakuweka katika nafasi nzuri ya kushinda.

“Lakini pia itapunguza mambo mengi, mfanyabiashara ataonana na mfumo, haonani na mtu hadi atakapokuja kukabidhi. Hapa Kwimba umenisaidia kwa sababu bei ya bidhaa nyingi imeshuka baada ya kuanza kutangaza ndani ya wilaya na nje ya wilaya. Umenisaidia hata malalamiko yamepungua ile ya kusema kila kazi anapewa fulani sasa hivi hayapo,” amesema.

Mkuu wa Idara ya Elimu ya Awali na Msingi wilayani Bunda, Oscar Kapinga amesema mfumo huo utaleta ufanisi kwa kuwa hata wazabuni hawana haja ya kutoa kitu au kupitia kwa mtu wa kati ili kujipatia zabuni za Serikali.

“Mfumo huu hauachi power (mamlaka) zote kwa Ofisa Manunuzi, lakini kwa sasa unakwenda mpaka kwa wazabuni wenyewe, kwa hiyo wanaelewa kumbe hakuna sababu ya kupitia kwa mtu mwingine ili wapate zabuni za Serikali, badala yake wanakwenda kwenye mfumo wanaomba tenda hamna mtu ambaye anaweza akapitia ili wamshawishi apate ile kazi,”amesema

Akizungumza kwenye mafunzo hayo, Meneja wa Kanda ya Ziwa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Juma Mukoja amewataka watumishi kuhakikisha manunuzi yote yanapitia kwenye mfumo huo ili kupata thamani halisi ya fedha.

“Sheria mpya hii ya 2023 kuna kifungu ambacho kimewekwa mahususi kabisa kwamba ofisa masuuli ambaye hatatumia mfumo kwenye manunuzi, atashitakiwa na anaweza kufungwa na kulipa faini,” amesema.

Amesema baada ya kutembelea halmashauri zote za Kanda ya Ziwa walibaini watumishi wengi wana uelewa mdogo kuhusu mfumo huo.

Kwa mujibu wa kifungu cha 106 (6) ya sheria ya utumishi wa umma ya mwaka 2023, mtumishi yeyote wa taasisi nunuzi, anayejihusisha na vitendo vya rushwa au udanganyifu wakati wa mchakato wa ununuzi au utekelezaji wa mkataba unaogharamiwa kwa fedha za umma atachukuliwa hatua, kwa mujibu wa masharti ya sheria hiyo.