DED mstaafu aangushwa uchaguzi wa CCM Bukombe

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Matondo Lutonja akitoa shukrani kwa wajumbe 655 katika baada ya kushindwa Picha na Ernest Magashi.

Muktasari:

Kelvin Makonda aliyewahi kuwa DED wilayani Bukombe ameshindwa uchaguzi kwa kuambulia kura 30 dhidi ya mpinzani wake Matondo Lutonja aliyepata kura 454.

Bukombe. Mkurugenzi mstaafu wa Wilaya ya Bukombe, Kelvin Makonda ameangushwa katika uchaguzi wa CCM alipokuwa akigombea nafasi ya uenyekiti wa wilaya hiyo kwa kuambulia kura 30, huku mshindi Matondo Lutonja akipata kura 454.

Akitangaza matokeo hayo leo Oktoba 3 saa 8:2 usiku, msimamizi wa uchaguzi wa wilaya hiyo, Jamhuri William amemtaja mgombea mwingine kuwa ni Robart Wanka aliyepata kura 173, huku kura zote zilizopigwa zikiwa 655 na iliyoharibika ni moja.

Amewaomba wanachama kuungana ili kukijenga chama kinacho shika dola.

"Naomba wanachama kushikamana tukijenge chama ili kuendelea kushika patamu," amesema.

Kwa upande wake mshindi wa uchaguzi hui, Matondo Lutonja amewaomba wajumbe kuungana kukijenga chama hicho.

"Uchaguzi umeisha, nawaomba tuungane kukijenga chama kwa kushirikiana na viongozi waliochaguliwa usiku wa kuamkia Oktoba 3, 2022," amesema Lutonja.

Wakizungumza katika uchaguzi huo, Wanka na Makonda wameahidi kumuunga mkono William.

Naye Mbunge wa jimbo hilo, Dk Doto Biteko amewaomba wanachama kumuunga mkono mwenyekiti aliechaguliwa na wavunje makundi ili kuendeleza maendeleo yaliyo anzishwa na viongozi waliopita.