Dereva aliyehusika na ajali ya Mwana-FA atibiwa chini ya ulinzi

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia dereva wa gari ndogo aina ya Crown (jina linahifadhiwa) iliyohusika na ajali iliyomhusisha Mbunge wa Muheza, Hamis Mwinjuma maarufu Kama Mwana FA iliyotokea eneo la Mkambarani, barabara kuu ya Morogoro-Dar es Salaam jana.

Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia dereva wa gari ndogo aina ya Crown (jina linahifadhiwa) iliyohusika na ajali iliyomhusisha Mbunge wa Muheza, Hamis Mwinjuma maarufu Kama Mwana FA iliyotokea eneo la Mkambarani, barabara kuu ya Morogoro-Dar es Salaam jana.


Mbalina Mwana FA aliyejeruhiwa, watu sita waliokuwa kwenye magari hayo nao walijeruhiwa.


Akizungumza kwa simu na Mwananchi leo Agosti 31, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Fortunatus Musilimu, amesema dereva huyo anaendelea na matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro chini ya ulinzi wa Polisi.


Amesema dereva huyo anatuhumiwa Kuwa chanzo cha ajali hiyo, baada ya kuharibu kulipita gari jingine lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari na kukutana na gari iliyokuwa imembeba Mbunge huyo wa Muheza na kugongana nalo na magari hayo kupinduka.


SACP Musilimu amesema ajali hiyo ilitokea August 30 majira ya saa 1 usiku katika eneo la Mkambarani.


Mbunge Hamis Mwinjuma akizungumza katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro baada ya Ajali, amesema yuko salama isipokuwa alikuwa na maumivu kidogo maeneo ya kifuani, na alikuwa akisubiri vipimo zaidi vya X-ray kuona Kama kuna tatizo zaidi.


"Hadi nimetoka kuzungumza hali yangu ni nzuri, na kwenye gari nilikuwa na dereva wangu ambaye amepata michubuko kidogo," alisema Mbunge huyo.


Akasema alikuwa akitokea Msoga nyumbani kwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ambaye alipatwa na msiba na alikuwa akielekea bungeni Dodoma.


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela aliyefika hospitalini hapo kuwajulia hali majeruhi, licha ya kutoa pole akavitaka Vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza na kubaini chanzo cha ajali ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa.