Diplomasia imara fursa kwa Watanzania kueneza Kiswahili

Muktasari:

Uhusiano mzuri na mataifa mengine unatajwa kuwa fursa muhimu ya kueneza na kukuza lugha ya Kiswahili na kutengeneza ajira kwa Watanzania wengi katika mataifa ambayo lugha hiyo inafundishwa.

Dar es Salaam. Kufunguka kwa diplomasia ya Tanzania kumetajwa kuwa fursa muhimu ya kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili ulimwenguni kote kwa kuifanya kuwa bidhaa inayotoka katika taifa hili.


Hayo yalibainishwa jana Desemba 8, 2022 mkoani Dar es Salaam wakati wa kongamano lililofanyika katika Chuo cha Diplomasia likijadili kuhusu miaka 61 ya uhuru na diplomasia ya Tanzania.


Akiwasilisha mada katika kongamano hilo, mhadhiri katika chuo hicho, Denis Konga alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameimarisha diplomasia ya Tanzania na mataifa mengine kupitia ziara zake, jambo ambalo linatengeneza fursa nyingi.


Alisema moja ya fursa hizo ni kuenea kwa lugha ya Kiswahili duniani na kukifanya kuwa bidhaa inayotoka Tanzania ambayo inatoa fursa nyingi kwa Watanzania ikiwemo kufundisha lugha hiyo ughaibuni.

“Moja ya fursa za kufunguka kwa demokrasia ni matumizi ya lugha ya Kiswahili. Mataifa mengine yameanza kutumia lugha hiyo na tayari imekubaliwa katika jumuiya za kikanda kama lugha rasmi,” alisema.


Aliwahimiza Watanzania kutafuta fursa za kimasomo zinazopatikana katika mataifa mengine ili kuimarisha maarifa yao na kujiongezea uwezo wa kushindana na wengine duniani.


“Kuna fursa za diaspora, tunawatumiaje hawa diaspora? Kuna fursa za masomo, vijana tafuteni fursa za maosomo. Lakini huwezi kutumia fursa hiyo kama hujafanya vizuri huku chini,” alisema Konga.


Kwa upande wake, mwanafunzi wa mwaka wa tatu, Lauden Kamyanda alisema Tanzania haijakipa Kiswahili kipaumbele, jambo ambalo limewafanya watu wengi kutoijua lugha hiyo kwa ufasaha.


“Sisi Watanzania wenyewe ambao tunajivunia lugha hii bado hatujaijua vizuri, hatujaipa kipaumbele. Sasa tutawezaje kuwafundisha wengine huko nje wakaijua?” alihoji mwanafunzi huyo.


Mwanafunzi mwingine, Frank Mpolani alisema Mwalimu Julius Nyerere alibainisha mambo manne muhimu katika maendeleo ambayo ni ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Alisema mambo mawili ya ardhi na watu tayari yapo lakini vinavyokosekana ni siasa safi na uongozi bora.


“Tunahitaji siasa safi na uongozi bora ili tuweze kupata maendeleo tunayoyahitaji. Tunahitaji kupiga hatua zaidi ya hapa, miaka 61 ya uhuru tumejifunza mengi na tunatakiwa tuboreshe,” alisema.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Utawala wa Chuo cha Diplomasia, Dk Jacob Nduye alisema Watanzania wana fursa nyingi lakini hawawezi kushindana na wenzao wa Kenya kwa sababu hawana utamaduni wa kusoma.


“Hatuna utamaduni wa kusoma ili kujiongezea maarifa, ndiyo maana wenzetu wanachukua fursa zetu. Watanzania tujenge utamaduni wa kusoma ili tupate nguvu ya kushindana na wengine,” alisema