Diwani ajivunia shule zake kuongoza kwa ufaulu Simanjiro

Muktasari:

  • Diwani wa Kata ya Endiamtu wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara, Lucas Zacharia amewataka wazazi na walezi kuchangia chakula shuleni kwani kinasababisha wanafunzi kusoma kwa bidii na kufaulu.


Simanjiro. Diwani wa Kata ya Endiamtu wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara, Lucas Zacharia amewataka wazazi na walezi kuchangia chakula shuleni kwani kinasababisha wanafunzi kusoma kwa bidii na kufaulu.

Zacharia akizungumza na wadau wa elimu baada ya kutembelea shule za kata yake, amesema kuwepo chakula shuleni kumsababisha wanafunzi wote 452 waliofanya mtihani kufaulu.

Amesema wazazi na walezi wanapaswa kuwaunga mkono walimu ili wafundishe ipasavyo na kuchangia chakula shuleni ili wanafunzi wasisome wakiwa na njaa.

"Kufaulisha wanafunzi 452 siyo jambo dogo kwani hakuna kata kwenye wilaya ya Simanjiro iliyofaulisha watoto wengi hivyo, tunapaswa kuwapongeza walimu," amesema Zacharia.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mirerani, Tenisia Katukuru amesema kati ya wanafunzi 103 waliojiandikisha kufanya mtihani ni wanafunzi 101 waliofanya na kufaulu wote.

Mwalimu Katukuru amesema wanafunzi hao wamefaulu wote darasa zima kujiunga na sekondari na wamejiandaa kwa mwaka huu kufaulisha zaidi.

Mmoja kati ya wazazi wanaosomeshaa wanafunzi kwenye shule ya msingi Mirerani, Yusuf Ali amesema anashangazwa na wazazi ambao wanashurutishwa kuchangia fedha ya chakula.

"Kuchangia chakula shuleni inakuwa ajenda ya kujadili ili hali hata akiwa nyumbani ni lazima ale chakula sasa unataka nani akulishie mtoto wako kama siyo wewe mwenyewe? amehoji.

Kata ya Endiamtu ina shule saba za msingi zikiwemo tatu za serikali na nne za binafsi.