Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Abbas awafunda maofisa habari serikalini

Muktasari:

Watendaji hao wanakutana jijini Arusha katika mkutano wao mwaka

Dar es Salaam. Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbas amewataka maofisa habari na mawasiliano wa Serikali kuwa imara, kusimamia ushauri wanaoamini na misingi ya taaluma yao  bila kusahau kujikita kwenye ukweli.

Dk Abbas aliyewahi kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo,  amesema hakuna sababu ya maofisa habari kulalamikia nafasi zao kwenye taasisi,  kwa kuwa utendaji wao ndiyo utakaothibitisha ni kwa kiasi gani wana umuhimu na kazi kubwa ya kufanya katika suala zima la mawasiliano.

Amesema hayo leo Jumanne, Februari 27, 2024 wakati wa mkutano wa mwaka wa Chama cha Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) jijini Arusha, alipokuwa akizungumzia uzoefu wake  kama mtaalamu wa mawasiliano  na jinsi ya kukabiliana na changamoto.

Dk Abbas pamoja na Mkurugenzi wa Uchechemuzi wa shirika la Twaweza Afrika Mashariki, Anastazia Rugaba walitoa uzoefu wao kukabiliana na changamoto ambazo maofisa habari hao wanafanyia kazi. Mjadala huo uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu.

Katika maelezo yake, Dk Abbas alisema kuna umuhimu mkubwa kwa maofisa habari na wasemaji wa taasisi kuwa makini wanaposhughulikia changamoto au majanga yanapojitokeza kwenye taasisi zao na kusimama kwenye misingi ya taaluma.

“Kila crisis (changamoto) ni somo kwa taasisi, kwamba taasisi kama inataka kukua au kuongeza mwonekano kwake kwa jamii ni lazima ipitiie na mkiifanya kuwa somo itasaidia kuipeleka hatua moja mbele. Kwenye changamoto uwe unaenda na hisia, kama ni eneo unalazimika kulia lia kwelikweli kwenye mkutano na waandishi ila kama hulazimiki usifanye hivyo,” amesema Dk Abbas

Ametolea mfano kile alichokifanya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni Ndege ya Precision Air Patric Mwanri, alipolia mbele ya waandishi wa habari wakati akizungumzia ndege yake iliyokuwa imeanguka Ziwa Vikctoria, Bukoba mkoani Kagera, Novemba 6, 2022.

Ndege hiyo iliyoanguka kando ya Uwanja wa Ndege wa Bukoba, ilisabaisha vifo vya watu 19 na majeruhi 26.

“Kuna eneo unalazimika kuwa jasiri. Nitolee mfano lile suala la  Precision Air hadi leo inabaki taswira ya yule CEO alilia mbele ya vyombo vya habari, lakini kama mnakumbuka wakati ule anatoa chozi kulikuwa hakuna taarifa yoyote ya kifo.

Sisi  wachambuzi wa mambo alivyolia tu nilijua watu wameshakufa, wakati mwingine hisia unazoonesha zinaweza kutoa mambo ambayo kwenye mkakati wenu hayakutakiwa kusemwa kwa wakati huo,” alisema Dk Abbas.

Akijibu hoja ya maofisa habari kutohusishwa kwenye baadhi ya mikutano ya uamuzi ndani ya taasisi au mashirika ya Serikali, Dk Abbas alisema ofisa habari siku zote anapaswa kuwa na kiherehere na inapolazimu kukataa kufanya jambo kwa sababu ya kutokuwa na taarifa za kutosha asisite kufanya hivyo.

Katika hilo alitolea mfano namna ambavyo janga la tetemeko la ardhi mkoani Kagera lilivyomuwezesha kupata gari lake la kwanza kama Msemaji Mkuu wa Serikali kufuatia kuonesha kwake msimamo akisimamia misingi ya taaluma yake.

“Mimi gari ya kwanza kupewa na Serikali kwa maana ya Msemaji Mkuu wa Serikali sasa ana gari rasmi la kulitumia, ni changamoto ya tetemeko la ardhi Kagera. Serikali ilipigwa karibu wiki moja, inachapwa tu kwamba haijasaidia watu.

Inafanya nini watu wanauliza msemaji yuko wapi mbona hasemi. Swali langu la kwanza lilikuwa nasemea nini, mimi sipo Kagera, sijui juhudi ya kinachofanyika huko watu wote walioweza kuwahi wamepewa magari, wamepewa posho wapo Kagera halafu mtu wa kusimamia uko Dar es Salaam,” alisema Dk Abbas na kuongeza

“Nilipoulizwa nilisema nipo Dar sina uwezo wala njia yoyote ya kwenda Kagera, kwa hiyo na mimi nazingatia misingi ya taaluma yangu siwezi kutunga stori kwamba Serikali inafanya nini huko Kagera wakati sipo huko. Hivi ndiyo ikawa fursa yangu ya kupewa gari.”

Naye Anastazia amewataka maofisa habari kuwa tayari kutengeneza mikakati ya mawasiliano na kuhusisha kipengele cha kukabiliana na majanga yanapotokea.

Pia, ameshauri kuona umuhimu wa kufanya kazi na sekta binafsi kwa kuwa kuna fursa nyingi ambazo taasisi na mashirika ya Serikali yanazikosa kwa kujiweka mbali na wadau wa sekta binafsi.

“Mtu wa mawasiliano ni lazima uwe king’ang’anizi, fanya kila unachoweza, hakikisha unasukuma hadi kupata kile unachokitaka. Kwa kufanya hivi ndiyo unaonesha uwepo wako na utaweza kubadilisha mambo,”amesema.

Awali, akifungua mkutano huo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro,  amewataka maofisa habari kuwa wazalendo na kutumia taaluma zao kuipambania Serikali na kutangaza miradi ya kimkakati. 


“Nikitolea mfano wa sakata la Ngorongoro aliyekuwa anapigwa sio Ngorongoro wala Wizara ya Maliasili na Utalii bali Serikali. Sasa nyie ndio maofisa habari wa Serikali lakini mlikaa kimya. Tunasisitiza kufanya kazi kwa pamoja kama timu, jambo likitokea ni la kwenu nyote mnachotakiwa kupata ni taarifa,” amesema


Jambo likitokea kwenye taasisi au wizara moja kupitia chama hiki ni la kwenu wote mshambulie wote, huko kwenye mitandao atakayejaribu kunyanyua shingo aone mvua ya mashambulizi kutoka kwa wataalam,” alisema Dk Ndumbaro .


Ametumia fursa hiyo kuwakumbusha maofisa habari kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu akiwataka kutoa taarifa za utendaji wa Serikali ili kuongeza imani ya wananchi.