Dk Hamis Kigwangalla : Msimamo wangu kuhusu tiba ya corona

Wednesday April 07 2021
maonipic

Dk Hamisi Kigwangalla

Juzi nilialikwa na kushiriki kwenye mdahalo wa ‘Zoom’ ulioandaliwa na Nadj Media Center. Mjadala ulikuwa mzuri na mkali sana.

Kwa kuanzia nataka ieleweke kuwa nilichokisema hakina lengo la kufubaza heshima (legacy) ya mtazamo/msimamo wa hayati Rais John Magufuli hata kidogo.

Niliunga mkono sera na utendaji wake akiwa waziri, akiwa Rais na siku zote nitazienzi fikra zake, hata baada ya kufa kwake.

Siyo kwa sababu aliniamini na kuniteua kuwa waziri kwenye serikali yake, la hasha, bali ni ukweli kwamba mimi ni miongoni mwa watu wachache waliopenda sera, staili na mwenendo wa hatua alizokuwa akichukua Rais Magufuli. Na nilimuunga mkono kwa vitendo kwa sababu nilimkubali na kumuamini kutoka moyoni.

Kwa kuwa nilikuwa na ‘access’ naye, sehemu ilipotokea nikawa na mawazo mbadala, sikusita kumshauri bila unafiki wala kujikomba.

Februari 6, 2021 niliweka posti kwenye mtandao wa IG iliyoelezea mashaka yangu juu ya chanjo ya corona. Nilisema ni mapema mno kuwa na uhakika nayo kwa kuwa hakuna ‘peer reviewed scientific papers’ (maandiko ya kisayansi yaliyochapishwa kwenye majarida ya kimataifa) ya kuridhisha juu ya usalama wa chanjo, uhakika kuwa chanjo zinasaidia kuzuia maambukizi (efficacy) na gharama yake (cost).

Advertisement

Siku saba baadaye nilipata makala ya chanjo ya corona kutoka Urusi, Sputnik V, iliyochapwa kwenye jarida la The Lancet. Niliisoma na kupata ‘mwangaza mpya’.

Februari 22, 2021 nilitoa makala juu ya mtazamo wangu kubadilika juu ya chanjo. Kwenye sayansi inakubalika kubadili msimamo wako kama umepata taarifa mpya ama ujuzi/ufahamu mpya.

Aidha, nilichukua muda kujadiliana na manguli wenzangu juu ya taarifa za chanjo na uelekeo sahihi kwa nchi yetu. Ifahamike kuwa wimbi la kwanza halikusumbua Afrika, la pili tulitarajia litusumbua zaidi kutokana na ‘mutations’ za kirusi.

Mimi kama daktari mbobezi kwenye afya ya jamii, niliamua kuweka wazi juu ya fursa mpya ya uhakika ya kinga iliyojitokeza kutokana na ujio wa chanjo.

Nilichokisema juzi kwenye mdahalo wa kitaalamu ni msimamo wangu wa kisayansi na niko tayari kuutetea na kuulinda kwa hoja za kisayansi popote pale.

Kwa kusoma ama kusikia vipande vilivyopo mtandaoni, huwezi kuelewa vizuri ni nini hasa msingi wa hoja zangu.

Hivyo, nawataka wanaopambana kugeuza maana halisi ya nilichoongea kwa sababu zao waache mara moja, na pia niwasihi wasihusishe na kauli ama msimamo wa mpendwa wetu hayati John Pombe Magufuli.

Msimamo wangu juu ya chanjo niliutoa kabla Rais Magufuli hajafariki, hivyo hakuna usaliti wowote ule ‘eti kwa kuwa ametangulia mbele ya haki. Sina tabia ya unafiki hata kidogo na hayati alinijua hivyo.

Aidha, kuhusu matumizi ya njia za kitaalamu za kujikinga, msimamo wangu ni uleule, haujabadilika. Kwamba, ni lazima tutumie njia za kuvaa barakoa kwenye mikusanyiko, kuweka nafasi kati ya mtu na mtu, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kutakasa mikono kwa maji tiririka na sabuni ama kwa sanitizer (vitakasa mikono) na kutoa chanjo kwa makundi muhimu.

Siyo ustaarabu kumsingizia marehemu kwa kuwa hawezi kutoa ufafanuzi tena ama kujitetea, kwa kutaka kujiita wazalendo ama kuonekana wewe ni mfuasi halisi wa Magufuli, na kwamba wengine ni wasaliti. Tudumu kwenye ukweli na tumpe mpendwa wetu sifa zake stahiki na siyo kumsingizia mambo.

Rais Magufuli katika uhai wake alisisitiza njia zote tunazoelekezwa na wataalamu zitumike. Alikataa kujifungia (lockdown) na alitaka tutumie barakoa zetu wenyewe, za kujishonea ama za viwanda vya ndani.

Aliielekeza Wizara ya Afya waitazame chanjo na wzara ya ikaunda kamati ya kitaalamu kufanya tathmini ya chanjo.

Hata hivyo, msimamo wangu uko palepale, kuwa tiba ya asili inaweza kutumiwa na daktari wa tiba na kwamba siyo sahihi kwa hospitali ya Taifa kutumia tiba ya asili bila ushahidi unaotokana na tafiti za kisayansi.

Hata kama tunaitambua na kuihamasisha, lakini siyo kuitangamanisha kwenye mfumo wa tiba za kisasa (zenye ushahidi wa kisayansi)!

Binafsi nimekuwa nikihamasisha utamaduni wetu utumike kiutalii, na ndiyo maana nilipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, nilihamasisha matumizi ya nyungu na zile dawa za kiasili kiutalii, lakini haimaanishi ndiyo naamini asilimia 100 kuwa zinatibu corona.

Nilisema siku nyingi na narudia tena leo, kuwa tujenge utamaduni wa kujadili hoja kwa namna ilivyo na siyo ku-attack personality (kumshambulia mtu) ya mtu ama kufumbana midomo.

Dk Hamisi Kigwangalla ni daktari bobezi wa afya ya jamii.

Advertisement