Dk Kiboro: Kusi Festival imeleta soko la usafiri wa anga Afrika

Kiboro: Kusi Festival imeleta Soko la Usafiri wa Anga Afrika

Muktasari:

Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Nation Media Group (NMG), Dk Wilfred Kiboro amesema zaidi ya nchi 17 za Afrika zimekubali na kuunga mkono mpango wa kuwa na ‘Soko la Usafiri wa Anga la Afrika (SAATM)’.

Nairobi. Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Nation Media Group (NMG), Dk Wilfred Kiboro amesema zaidi ya nchi 17 za Afrika zimekubali na kuunga mkono mpango wa kuwa na ‘Soko la Usafiri wa Anga la Afrika (SAATM)’.

Hayo ameyasema leo Alhamisi Desemba 8, 2022 wakati akizungumza kwenye tamasha la ‘Kusi Ideas Festival’ lililoandaliwa na NMG linalofanyika Nairobi nchini Kenya.

“Tangu tuanzishe tamasha hili, tunafarijika kuona baadhi ya mawazo yetu yanaungwa mkono na karibia bara zima la Afrika kwa mfano mwaka 2019 tamasha kama hili tulilifanya Kigali (Rwanda) na moja ya wazo lilikuwa kufungua kwa anga la Afrika ‘The Single African Air Transport Market (SAATM), kitu ambacho kimeungwa mkono sana,”amesema.

Pia, Kiboro amesema malengo ya kuanzisha kwa tamasha hilo ni pamoja na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazolikabili bara la Afrika.

“NMG ilianzisha tamasha hili 2019 likiwa na malengo makuu matatu; kwanza kuiandaa Afrika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili, kuchochea uanamajui wa Afrika kwenye kujadili changamoto zake zenyewe na kuchangia kutafuta na kutambua nafasi ya bara letu la Afrika duniani,” amesema.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango ameshiriki tamasha hilo lenye kaulimbiu inayosema “Mabadiliko ya Tabianchi: Kuchunguza Majibu na Suluhu za Kiafrika” kwa njia ya video.