Dk Kijaji ataja maeneo ya kuchochea mageuzi mifugo na uvuvi 2025/2026

Muktasari:
- Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka Sh295 bilioni kwa mwaka wa fedha 2023/2024 hadi Sh476.6 bilioni kwa mwaka huu wa 2025/2026.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji amewasilisha bajeti hiyo ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 huku akieleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Pia ameeleza hatua mbalimbali za kimkakati zilizochukuliwa na wizara hiyo katika kuhakikisha lengo la kuziwezesha sekta hizo muhimu kuendelea kuwa na mchango zaidi kwenye Pato la Taifa (GDP), linafanikiwa.
Bajeti hiyo iliyowasilishwa leo Ijumaa, Mei 23, 2025 bungeni mjini Dodoma, imetoa mwelekeo wa kuongezeka kwa uzalishaji na kukuza masoko ya mazao ya mifugo na uvuvi.
Dk Kijaji amesema katika kuhakikisha malengo yote ya kimkakati yanafikiwa, Serikali imeongeza bajeti ya wizara hiyo kutoka Sh295 bilioni kwa mwaka wa fedha 2023/2024 hadi Sh476.6 bilioni kwa mwaka huu wa 2025/2026.
“Hatua hii inadhihirisha dhamira ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha sekta za mifugo na uvuvi zinaendelea kuwa chachu ya uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja,” amesema Dk Kijaji.
Amesema kuwa utekelezaji wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) imewezesha vikundi 20 vyenye vijana 106 kupatiwa ekari 1,761 katika Ranchi ya Kagoma na kupewa mkopo usio na riba wa Sh934 milioni kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
Mkopo huo unalenga kuendesha shughuli za unenepeshaji ng’ombe, ambapo vijana hao walianza kazi ya unenepeshaji wa ng’ombe Januari, 2025 na hadi kufikia Aprili, 2025 jumla ya ng’ombe 627 wenye thamani ya Sh451 milioni walinunuliwa na kunenepeshwa.
Tayari kupitia mpango huo, vijana waliojikita kwenye kuendesha shughuli za ufugaji wa kisasa wameendelea kuwezeshwa kwa fadha na mafunzo ya namna bora ya kuendesha shughuli ili kuongeza tija.
Akizungumzia kupumzishwa kwa shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika, Dk Kijaji amesema umekuwa na manufaa makubwa kwa mataifa yote huku kwa Tanzania mavuno ya samaki yameongezeka hadi kufikia tani 38,999.82 katika kipindi cha miezi minne baada ziwa hilo kufungwa kati ya Septemba hadi Desemba, 2024 ikilinganishwa na tani 25,113.43, za awali.
Kutokana na ongezeko hilo, mazao ya uvuvi yaliyouzwa nje ya nchi kutoka Ziwa Tanganyika kwa mwaka 2024 yameongezeka na kufikia tani 1,227.21 ikilinganishwanatani 664.11 kwa mwaka 2023.
Kwa mujibu wa Dk Kijaji, mafanikio mengine yaliyopatikana kwenye wizara hiyo ni kudhibiti na kukomesha uvuvi haramu wa kutumia vilipuzi katika Ukanda wa Bahari ya Hindi.
“Kwa sasa hali ni shwari kabisa, hakuna tena tishio kama ilivyokuwa hapo nyuma baada ya wahalifu hawa kudhibitiwa. Tumedhibiti kuanzia vyanzo, wasambazaji na watumiaji wa vilipuzi na kwa zaidi ya mwaka hakuna matukio ya uvuvi huo kwa ukanda wote wa Bahari ya Hindi,” ameongeza Dk Kijaji.
Pia, amesema katika kuhakikisha hilo halijitokezi tena, wizara yake imeweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji huku akibainisha kuwa wameendelea na kasi ya kusafisha na kuondoa zana haramu za uvuvi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji amewasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026 jijini Dodoma leo Mei 23, 2025
Amesema mikakati hiyo inatekelezwa kupitia ushirikishwaji thabiti wa wadau mbalimbali wa sekta hiyo wakiwemo viongozi wa Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi na Asasi Zisizo za Kiserikali (NGOs).
Mikopo ya vizimba vya samaki
Katika hatua nyingine, Dk Kijaji amesema wizara hiyo imeendelea na utekelezaji wa mradi wa kutoa mikopo isiyo na riba na yenye masharti nafuu wa kuwezesha wananchi kupata vizimba vya kufugia samaki na pembejeo. Wananchi walionufaika ni mpango huo ni kutoka mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza, Kagera, Geita, Katavi, Rukwa na Kigoma huku akibainisha kuwa hadi kufikia Aprili 2025 vizimba 480 vimekopeshwa kwa wanufaika 1,338.

Pia, amesema kwa mara ya kwanza, Serikali inakwenda kuzindua na kutekeleza kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo nchi nzima lengo likiwa ni kuboresha afya ya mifugo na kuiongezea thamani ili iweze kuuzika kwenye masoko ya kimataifa.
Mauzo ya nyama yazidi kupaa
Wakati uboreshwaji wa mifugo ukiendelea katika maeneo mbalimbali nchini, Dk Kijaji amelieleza Bunge kuwa Serikali kupitia Bodi ya Nyama imeendelea kutekeleza mkakati wa kukuza mauzo ya nyama nje ya nchi kwa ajili ya kuongeza fedha za kigeni.
Amesema nyama ya Tanzania imendelea kuwa na masoko ya uhakika nje ya nchi na kwamba, hadi kufikia Aprili 2025 jumla ya tani 9,863.41 za nyama zenye thamani ya Sh3.7 trilioni ziliuzwa.
Awali, Tanzania ililenga kuuza tani 10,971 za nyama ikilinganishwa na tani 9,326.3 zilizouzwa kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha 2023/2024. Ongezeko hilo linatajwa ni jitihada za Rais Samia kuongeza ushirikiano na fursa za kibiashara nje ya mipaka ya Tanzania.

Kwa sasa Tanzania inapeleka nyama kwenye nchi za Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Vietnam.
Kuhusu ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ambayo wizara yake unaendelea kuutekeleza, Dk Kijaji amesema ujenzi wake umefikia asilimia 81.9. na kwamba tayari ajira 570 zimetengenezwa huku itakapokamilika itakwenda kuajiri zaidi ya watu 30,000.