Dk Kijazi awataka maofisa habari kutoa elimu ya sensa kwa umma

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Allan Kijazi

Muktasari:

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Allan Kijazi amewataka maofisa Habari na Mawasiliano Serikalini kuhakikisha wanatoa elimu kwa umma kuhusu Sensa ya Makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti 2022.

Tanga. Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Allan Kijazi amewataka maofisa Habari na Mawasiliano Serikalini kuhakikisha wanatoa elimu kwa umma kuhusu Sensa ya Makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti 2022.

Dk Kijazi amesema hay oleo Alhamisi wakati akizungumza na maofisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikalini wanaofanya kikao chao cha 17 jijini Tanga.

Amesema "Hii ni mara ya kwanza kwa sensa ya aina hii (nyumba) kufanyika katika nchi yetu,"

Amesema kuwa sensa hiyo inalenga kulipatia taifa hifadhi ya data ya Makazi ambayo itaiwezesha Tanzania kuwa na mikakati sahihi ya makazi.

Dk Kijazi amesema kuwa sensa ya nyumba ni muhimu katika kuifanya Serikali kuelewa mchango wa Serikali katika maendeleo ya makazi, kuelewa ukubwa wa msongamano wa nyumba na itaiwezesha kufanya tathmini ya kina ya hali ya umiliki na usawa wa kijinsia katika umiliki wa nyumba.

"Hapa ninyi mna jukumu kubwa la kufanya kuelewa umuhimu wa sensa ya nyumba na kushiriki ili kufanikisha," amesema.

Wakati huo huo, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anna Makinda amewaonya watumishi wanaochukua rushwa kutoka kwa watumishi wa umma na watu wengine wanaotaka kuteuliwa kuwa makarani wa sense, akisema watachukuliwa hatua.

“Tumeanza kupokea simu na jumbe kutoka kwa watu wanaotafuta upendeleo. Wakati huu hakuna kitu kama kupendelea jamaa au marafiki. Tumetengeneza mfumo mzuri wa kutuma maombi mtandaoni ambapo ni wale tu walio na sifa zinazohitajika ndio watapata kazi hiyo,” amesema.

Makinda amesema wakati huu kumekuwa na tabia ya baadhi ya maofisa wa Serikali kuomba rushwa kwa watu wakiwemo watumishi wenzao kwa ahadi ya kurahisisha njia ya kuchaguliwa kwenye kazi hiyo.

Amewaonya wanaotaka kuchaguliwa kuzingatia utaratibu uliotolewa na Serikali kwa sababu watakuwa wanapoteza fedha zao kwa maofisa hao wakorofi.