Dk Mpango aeleza alivyoshikwa na butwaa alipopendekezwa kuwa makamu wa rais

Dk Mpango aeleza alivyoshikwa na butwaa alipopendekezwa kuwa makamu wa rais

Muktasari:

  • Makamu wa Rais mteule, Dk Philip Mpango amesema wakati Bunge likijiandaa kupokea jina la aliyeteuliwa kuwa makamu wa rais, alikuwa akihangaika na mambo mengine ikiwemo mishahara ya wabunge na  kwamba jina lake lilipotajwa alishikwa na butwaa.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais mteule, Dk Philip Mpango amesema wakati Bunge likijiandaa kupokea jina la aliyeteuliwa kuwa makamu wa rais, alikuwa akihangaika na mambo mengine ikiwemo mishahara ya wabunge na  kwamba jina lake lilipotajwa alishikwa na butwaa.

Waziri huyo wa Fedha na Mipango ameeleza hayo leo Jumanne Machi 30, 2021 mara baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kutangaza jina lake katika kikao cha kwanza cha Bunge la 12.

“Kwanza napenda kumshukuru Mungu kwa namna ya pekee kabisa kwa kutupatia uhai na kutuwezesha kukutana hapa ili kuendelea na shughuli zetu za kikatiba.”

“Pili napenda kumshukuru sana mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri jeshi mkuu kwa kupendekeza jina langu na kuridhiwa na chama chetu ili liweze kuletwa hapa,” amesema.

Huku akizungumza kwa umakini, “hii ni nafasi muhimu sana na nyeti ya makamu wa rais ni heshima kubwa sana sikuwahi kuota, wakati naibu wangu anajibu swali nilikuwa nahangaika kwenye mambo mengine ikiwemo mishahara ya baadhi ya wabunge, nimetoka nje mara kadhaa kujaribu kuhangaika lakini nimepigwa na butwaa.”

Dk Mpango alizaliwa katika wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma mwaka 1957. Alisoma shule ya msingi Kipalapala na Muyama, alijiunga seminari ya Ujiji na baadaye seminari ya Utaga Tabora. Alijiunga kidato cha tano na sita katika sekondari ya Ihungo, Bukoba na alihitimu mwaka 1977  na kujiunga na jeshi la kujenga Taifa.

Baada ya mjadala wa wabunge kuhusu uteuzi huo, wabunge watapiga kura kuthibitisha jina la Dk Mpango.