Dk Mpango ataka waandishi wawezeshwe kuandika mazingira

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akizungumza katika kongamano la wahariri na wadau wa uhifadhi, mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji lililoandaliwa na kituo cha wanahabari watetezi wa rasilimali na taarifa(MECIRA) linalofanyika leo Jumatatu Desemba 19, 2022 mjini Iringa.

Muktasari:

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema kutokana na taarifa alizopata kuhusu uharibifu wa mazingira katika bonde la Ihefu, kuna haja ya waandishi wa habari kuwezeshwa kuanbdika habari za mazingira.

Iringa. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ameitaka Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia mazingira kuandaa bajeti kwa ajili ya kuwapa mafunzo waandishi wa habari ili waweze kuandika habari za mazingira kwa ufasaha.

Mpango amesema hayo leo Desemba 19, 2022 mjini Iringa katika kongamano la wahariri na wadau wa uhifadhi, mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji lililoandaliwa na kituo cha wanahabari watetezi wa rasilimali na taarifa(MECIRA).

Dk Mpango amesema kuwa kutokana na taarifa alizopokea leo katika kongamano hilo, ipo haja ya wanahabari kuwezeshwa kufanya habari za uchunguzi na kupewa mafunzo.

 "Naomba Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia mazingira kutenga fedha kwa ajili ya waandishi kupewa mafunzo ya uhandishi wa habari za mazingira ili habari zitakazotoka zisiwe za ubabaishaji na uchonganishi," amesema.

 Dk Mpango pia amesema kuwa baadhi ya viongozi mbalimbali wamekuwa waharibifu wakubwa wa vyanzo vya maji na mazingira kwa shughuli za uchumi ambazo zina faida kwa watu wachache.

"Viongozi wa aina hiyo hawafai katika jamii hivyo Serikali haiwezi kuwafumbia macho watu kama hao ambao wanaangamiza jamii nyingine kwa makusudi.

"Madhara ya uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji yamekuwa makubwa na jamii inaathirika kiuchumi,kiafya hata kielimu kwa ajili ya watu wachache wanaoharibu mazingira," amesema Mpango.

Amesema kuwa bonde la Ihefu ni muhimili wa mabwawa ya Mtera, Kidatu na Mwalimu Nyerere, watakaohujumu upatikaji wa maji kutoka kwenye hilo bonde hatua kali zitachuliwa.

Ameitaka Mamlaka ya Bonde la Rufiji kwenda kubomoa mabwawa yote ambayo yanahifadhi maji kinyume na sheria na kuwataka wamepeleke vibali vyote vya matumizi ya maji walivyo vitoa ili aweze kuvitia na kujua vilitokaje.

Ameisema kuwa madhara yamekuwa makubwa sana kwani mwaka 1980 uharibifu ulikuwa asilimia 42,mwaka 2012 uharibifu ulikuwa asilimia 50 na mwaka 2018 uharibifu ulikuwa asilimia 63 hivyo hali inaendelea kuwa mbaya kila kukicha.