Dk Mpango: Mabadiliko tabia nchi yanaathiri uchumi wa Tanzania

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango

Muktasari:

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango amesema mabadiliko ya tabia nchi yameathiri ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuzorotesha shughuli za kiuchumi za wananchi zinazotegemea mazingira.

Nairobi. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango amesema mabadiliko ya tabia nchi yameathiri ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuzorotesha shughuli za kiuchumi za wananchi zinazotegemea mazingira.

Mpango, amesema hayo leo Alhamisi Desemba 8, 2022 wakati akichangia kwa njia ya video katika tamasha la Kusi lenye mada inayosema “Mabadiliko ya Tabianchi: Kuchunguza Majibu na Suluhu za Kiafrika” lililoandaliwa na kampuni ya NMG inayomiliki kampuni ya Mwananchi Communications Limited.

“Ni wazi kwamba athari za mabadiliko ya tabia nchi zinaathiri ukuaji wa uchumi wa nchi yetu hasa katika kuyafikia maendeleo stahimilivu na kupunguza umaskini kwa wananchi wetu.

 “Tanzania kama ilivyo nchi nyingine za afrika imeathirika na mabadiliko ya tabia nchi yanayoleta madhara kama vile mafuriko na ukame ambayo yanaathiri maisha ya jamii zote za mjini na vijijini,” ameongeza.

Aidha, Mpango amesema mabadiliko ya tabia nchi yaathiri Zaidi shughuli za kiuchumi ambazo ndio chanzo kikubwa cha Pato la Taifa

“Athari za mabadiliko ya hali ya hewa yanaathiri uzalishaji wa mazao ya kilimo, miundombinu, vyanzo vya maji na usambazi wa nishati, afya ya jamii na mfumo wa ikolojia,” amesema.

Akizungumzia mbinu ambazo Tanzania inatumia kukabiliana na changamoto hizo za mabadiliko ya tabia nchi mpango amesema,

“Serikali ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto hii kama ifuatavyo; kuhifadhi asilimia 40 ya ardhi yote maeneo ya pembezoni mwa bahari, tunapanda miti ambapo kila wilaya inapanda miti milioni 1.5 kwa mwaka.

“Pia tumeongeza uwekezaji kwenye nishati jadidifu ikiwemo umeme wa jua, joto ardhi na upepo, tumeanzisha kituo cha kuchunguza hewa ukaa, june 2022 tulizindua mpango madhubuti wa kutunza mazingira, tumezindua kampeni mbalimbali za kupinga matumizi ya nishati ya mkaa,” ameongeza.

Aidha, Mpango amesema katika kukabiliana na changamoto hizo mbali na kutumia njia bmbalimbali bado Tanzania inaamini sayansi, teknolojia na ubunifu vitasaidia kutatua kero hiyo.