Dk Mpango: Viongozi wa dini kemeeni ubakaji, ulawiti

Muktasari:

  • Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewaangukia viongozi wa dini akiwataka kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili katika jamii ikiwemo ubakaji na ulawiti akibainisha kuwa vitendo hivyo ni kama vinaanza kuonekana kuwa vya kawaida.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewaangukia viongozi wa dini akiwataka kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili katika jamii ikiwemo ubakaji na ulawiti akibainisha kuwa vitendo hivyo ni kama vinaanza kuonekana kuwa vya kawaida.

Dk Mpango ameeleza hayo leo Jumapili  Januari  29, 2023 katika ibada ya kumsimika Askofu Philipo Mafuja kuwa Askofu wa Kanisa la Afrika Inland Church Tanzania (AICT)Dayosisi ya Pwani.
“Nataka kurejea yale nilioongea na viongozi wa dini Novemba mwaka jana jijini Dar es Salaam, kukemea vitendo hivi ambavyo ni chukizo kwa Mungu na vinaenda kinyume na maadili yetu ya kitanzania.’’
“Matendo hayo ni pamoja na ubakaji, ulawiti, ushoga, ukahaba, matumizi ya dawa za kulevya, rushwa, ukatili na unyama dhidi ya wanawake na watoto wetu, ndoa na mimba za utotoni na matumizi ya mavazi yasiyo na staha.”
Akizungumza kwa msisitizo Dk Mpango amesema kuporomoka huko kwa maadili ni jambo lenye athari mbaya kwa jamii na Taifa na kunachangia kurudisha nyuma juhudi za kuharakisha maendeleo ya Tanzania.
“Lakini mimi naamini kwa dhati kabisa kama waumini wetu wakishika mafundisho ya dini vizuri maovu mengi yatapungua  na  pengine  kuisha kabisa na ndio maana kila nikipata fursa  kama hii narejea ombi langu kwa viongozi wa dini kwamba mtusaidie serikalini kujenga jamii yenye maadili mema.’’
“Pia kuweka mkazo haswa kwa vijana kwa kuwa wao ndio walengwa  wakuu wa maovu yanayotendeka lakini pia wao ndio warithi wa Taifa la leo na kesho .
Amesisitiza, “hivyo kama tukiwaandaa vizuri, mustakabali wa Taifa letu na watu wake utakuwa kwenye mikono salama lakini tukishindwa leo tutalia sana na kusaga meno na taifa letu litakuwa mashakani.”