Dk Mwaikali akabidhi kiti cha uaskofu

Wednesday June 22 2022
askofupiic
By Saddam Sadick

Mbeya. Aliyekuwa Askofu mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde, Dk Edward Mwaikali amekabidhi ofisi  na mali zote ikiwamo kiti cha uaskofu kilichokuwa kikipigiwa kelele na upande wa uongozi mpya chini ya Askofu Geoffrey Mwakihaba.

Makabidhiano hayo yalianza tangu Juni 14,2022 alipokabidhi baadhi ya mali ikiwamo magari 10, ambapo leo Jumatano Juni 21,2022 amekabidhi ofisi kwa ujumla lakini kiti cha uaskofu nacho kikibebwa kurudishwa makao makuu yaliyopo Tukuyu.

Tukio hilo lilianza saa 4 asubuhi na kumalizika saa 12 jioni, ambapo Jeshi la Polisi lilikuwepo eneo hilo kuimarisha usalama, huku baadhi ya waamini haswa wanaomuunga mkono Askofu Mwakihaba wakishudia shughuli  hiyo.

Shangwe na nyimbo kadhaa ziliimbwa kanisani wakati wakikinyanyua kiti cha uaskofu huku Mwakihaba akitumia muda mfupi kuwashukuru walioshirikiana tangu mwanzo hadi leo.

"Leo ilikuwa mwendelezo wa kukabidhiana mali, ambapo asilimia zaidi ya 90 tumepewa ikiwamo vifaa vya uaskofu kama pete, mkufu, kiti, ofisi, magari, pikipiki, mashamba ya miradi na nyumba walizokuwa wanatumia," amesema Mwakihaba.

Akizungumza baada ya kukabidhi mali wakili wa Askofu Dk Mwaikali, Wiliam Mashoke amesema wamekabidhi rasmi mali na ofisi na kuanzia leo haiko tena mikononi mwa Askofu Mwaikali na kuhusu mteja wake kuhamia Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki halijui.

Advertisement

"Kama mlivyoona leo tumekabidhi mali na haiko tena mikononi mwa Dk Mwaikali, ila warejee maandiko matakatifu, Luka 15 mstali wa 1-7 hasa wa nne," amesema Wakili Mashoke.

Advertisement