Dk Ndumbaro: Andikeni vitabu kutoa elimu

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro akishika kitabu cha Masuala muhimu ya Kazi na Ajira, kilichoandikwa na Wakili Ally Kileo (wa kwanza kushoto) jana Dar es Salaam. Wengine ni Profesa Chris Peter Maina na Kaimu mkurugenzi wa TLS, Mariam Othman.

Muktasari:

  • Amesema uandishi wa vitabu siyo kazi ya lelemama, kwani inamhitaji mwandishi kuwa mvumilivu na kuhakikisha anakusanya mambo yote muhimu anayotaka kuwafikishia wasomaji.

Dar es Salaam. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amewataka wanataaluma nchini kujenga tabia ya kuandika vitabu ili kutoa maarifa kupitia maandishi yao.

Ametoa wito huo jana Januari 25 alipokuwa akizindua kitabu cha ‘Masuala muhimu ya Sheria za Kazi na Ajira’ kilichoandikwa na Wakili Ally Kileo jijini hapa.
Amesema uandishi wa vitabu siyo kazi ya lelemama, kwani inamhitaji mwandishi kuwa mvumilivu na kuhakikisha anakusanya mambo yote muhimu anayotaka kuwafikishia wasomaji.

“Nawashauri Watanzania kujenga tabia ya kuandika ili kutoa elimu kupitia uandishi. Sheria za Ajira na kazi ni maeneo muhimu katika fani ya sheria ambayo wanasheria wanapaswa kuyaandikia,” amesema.

Amesema mbali na kitabu cha Kileo, ameshazindua vitabu vitano vya wanasheria, vikiwemo vya Profesa Zakayo Lukumay, Jaji Mlacha na Daudi Kinywafu na Dk Clement Mashamba.

“Kuandika kitabu hiki kikiwa na kurasa zaidi ya 800 siyo kazi rahisi, nikiwa kama mwanataaluma, mwandishi na mchapishaji, natambua ugumu aliopitia Kileo kufikia hapo,” alisema.

Akiwa Waziri anayehusika na masuala ya sheria, ambako Tume ya Kurekebisha sheria ya Tanzania iko chini yake, amewashauri kukisoma kitabu hicho ili kuona jinsi ya kuboresha sheria za kazi na ajira, ili kama kuna haja ya kubadilisha, Wizara, taasisi na wadau wengine wahusishwe.

Akikizungumzia kitabu hicho, Profesa wa Sheria, Chris Peter Maina amesema kimekuja kwa wakati kwani matatizo ya kazi na ajira ni makubwa nchini.

“Ibara ya 23 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inazungumzia haki ya mtu kupata ujira kwa kazi anayofanya. Hivi kweli Watanzania wanapata ujira sawa na kazi wanazofanya? Tunafuata kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi na sekta ya umma?” alihoji.

Amesema kitabu hicho kinazungumzia mapambano kati ya wafanyakazi na waajiri na kwamba kitabu hicho kinafafanua
Akizungumzia kitabu hicho, mwandishi na Wakili Ally Kileo amesema kwa muda mrefu alikuwa na ndoto ya kuandika kitabu cha kitaaluma na sasa ameitimiza.

“Niliota ndoto ya kuandika kitabu na leo nimeitimiza, nawashukuru sana kwa kuniunga mkono,” amesema Kileo.