Dk Slaa afunguka

Dk Slaa afunguka

Muktasari:

  •  Balozi wa Tanzania nchini Sweden anayemaliza muda wake, Dk Wilbrod Slaa, amesema suala la Katiba Mpya ni muhimu, lakini linahitaji maandalizi ya kutosha na ya msingi.


Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Sweden anayemaliza muda wake, Dk Wilbrod Slaa, amesema suala la Katiba Mpya ni muhimu, lakini linahitaji maandalizi ya kutosha na ya msingi.

Dk Slaa ameyasema hayo katika mahojiano yake na Mwananchi, ikiwa ni siku chache kabla ya kumaliza muda wake wa ubalozi nchini humo na kusema kuwa Katiba si jibu la kitu na Tanzania haiwezi kuacha kila kitu kwa ajili ya kuwa na Katiba Mpya.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini Ikulu Juni 28, Rais Samia aliulizwa kuhusu kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya, lakini alionyesha kuliweka kando suala hilo akisema kuwa kwa sasa anataka kupata muda wa kuimarisha uchumi.

Akizungumzia suala hilo la Katiba, Dk Slaa alisema: “Tusitegemee muujiza kwenye kitu kinachoitwa Katiba, lakini inataka maandalizi mazuri, tunachotaka kukifanya sasa ni zimamoto. Unaweza kuandaa kitu nusu nusu ukapata madhara. Lakini hayo majibu yangu hayamaanishi kuwa Katiba si muhimu.’’

Kuhusu mwenendo wa siasa za upinzani kwa sasa, Dk Slaa alisema, asingependa kubeba mzigo wa kushauri akiwa nje ya siasa, lakini hata hivyo, jambo la msingi kwa chama siasa ni kuwa na ajenda.

Dk Slaa ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa Chadema na mgombea wa urais kupitia chama hicho alisema, ili chama cha upinzaji kipendwe na wananchi hakina budi kuwa na ajenda zinazogusa umma.

“Mkienda kwenye ajenda zisigusa umma Watanzania hawatawatazama, hata kama mngekuwa na Katiba Mpya kesho,” alisema na kuongeza:

“Hili Taifa tunahitaji kulibeba wote, kila mmoja ana mchango wake unaohitajika; kila mmoja anatakiwa kurekebisha dosari zilizopo, robo tatu ya dosari zilizopo, lakini kila mmoja afanye kazi eneo lake.”

Dk Slaa alisema wapinzani nao ni Watanzania, lakini upinzani haupo Tanzania peke yake, hata nchi zilizoendelea zina upinzani.

“Hata nchi za Ulaya zina upinzani na bado zinapaza sauti kuhusu haki za binadamu, hivi wangapi mnajua Denmark iliwahi kupelekewa watunza amani’?” alisema.

Mwananchi lilimuuliza pia ikiwa bado ana nia ya kugombea urais, alisema:

“Hotuba yangu Septemba Mosi 2015 mnaikumbuka. Usitafute uchawi. Mimi ni mwanasiasa anayejua siasa, ambaye akishatoa kauli habadiliki habadiliki, labda kulingana na mazingira, sina nia ya kurudi katika ‘actual’ politics” (siasa majukwaani).

Kadhalika Dk Slaa alipoulizwa kuhusu maoni ya wadau kwamba demokrasia na haki za binadamu zinakandamizwa nchini hasa pale Jeshi la Polisi linapowazuia wafuasi wa vyama vya upinzani, huku likiwaruhusu wa chama tawala, Dk Slaa alisema msingi mkubwa ni kujua sheria na taratibu za nchi zinataka nini.

“Ni muhimu kujiuliza je, hii haki tunazolalamikia kwa wengine, je, mimi nipo sawa? Utanyoosha kidole kimoja kwa mwingine na vidole vitatu vinakugeukia wewe ni muhimu kama Taifa kutafuta mustakabali wa pamoja,” alisema

Alisema wakati akiwa kwenye siasa, Halmashauri ya Karatu, ilitaka kufutwa kwa barua, lakini hakufanya mgogoro wala kugombana bali kama chama waliangalia sheria inasema nini.

“Nafikiri kila mmoja akicheza vizuri mahali pake kwa umakini, mengine yote ya kuvurugana hayatakuwepo. Watanzania tujue haki zetu, tuna nafasi pana lakini hatuzitumii,” alisema

Dk Slaa aliongeza na kusema, hata bila Katiba Mpya wakati ule akiwa mbunge wa Karatu, alishirikiana na wananchi na kupigania haki iliyosababisha hiyo isifutwe.

Wanawake na uongozi

Kuhusu Rais Samia kuonyesha nia ya kugombea tena urais 2025, alisema:

“Ukitaka kunyanyua jinsia, ni suala lisilokuja kwa miujiza, hapa Tanzania mnaona ni jambo la ajabu lakini hapahapa Sweden, wanawake wanashika nafasi za juu, hata Finnland waziri mkuu ni mwanamke na Denmark waziri mkuu ni mwanamke.”

Dk Slaa alisema wanawake wameiva kwa kuwa katika nafasi za juu za uongozi, na kwamba Rais Samia ameiweka Tanzania katika ramani ya kimataifa.

“Mama alichosema, ni kwamba anatekeleza maazimio ya mkutano wa Beijing, kwa kuichukua ajenda ya miaka 20 iliyopita, tangu mwaka ule hatukupata mtu makini wa kumuunga mkono mama Getrude Mongela, lakini sasa Samia ametekeleza yale maazimio.”alisema

Pamoja na kugusia demokrasia, upinzani na masuala ya jinsia, aidha, Dk Slaa alizungumzia kile kinachosemwa na baadhi ya watu kuhusu tofauti ya uongozi kati ya Rais Samia na mtangulizi wake.

“Mama Samia ametembea katika nyayo za JPM.Kwa mfano, kuhusu chanjo ya Covid-19, ameunda timu ya watalaamu ambao walifanya uchunguzi kuhusu ubora na kujiridhisha kabla ya kuitumia,” alisema

Alisema hata hayati John Magufuli alisema ni muhimu kujiridhisha kwanza kwa kufanya utafiti kabla ya kuleta chanjo hiyo.

Kuhusu safari za nje ya nchi za Rais Samia, Dk Slaa alisema huo ulikuwa ni utaratibu uliokuwepo tangu awali kwa hayati Magufuli kufanya kazi za ndani, huku Samia akifanya za kidiplomasia.

“Mimi sijaona tofauti. Pia usisahau kuwa viongozi wawili hawatafanana kwa asilimia 100, iwe ni kwa kauli, kimtazamo , upole au ukali. Hata siku moja hawawezi kufanana kwa kila kitu,”alisema