Dk Tulia awalaumu viongozi serikali za mitaa kukithiri kwa uchafu jiji la Mbeya
Muktasari:
- Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amemuagiza ofisa usafi jiji la Mbeya, Nimrod Kiporoza kuanza leo Jumatatu Januari 2, 2023 kutokwenda ofisini mpaka akague maeneo yote ya jiji kujiridhisha hali ya usafi ilivyo na endapo kama kutakuwa na sababu ya magari atoe taarifa.
Mbeya. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema kukithiri kwa uchafu wa mazingira katika jiji la Mbeya ni kutokana na usimamizi mbaya wa madiwani na wenyeviti wa Serikali za mitaa ambao wamerejeshewa jukumu la uondoshaji wa taka katika maeneo yao.
Dk Tulia amesema leo Jumatatu Januari 2, 2023 mara baada ya kushiriki shughuli ya kuondoa mrundikano wa taka katika kata ya Ruanda jijini Mbeya huku kukiwa na mvutano baina ya diwani wa kata hiyo, Reuben Kipalule na wenyeviti.
“Hali sio salama kabisa na ikumbukwe suala la usafi ninalizungumzia kila siku sasa leo hii nimeshuhudia taka ambazo zimelalamikiwa na wananchi kukaa kwa muda mrefu kabla ya mzabuni kupewa tenda ya kuzoa taka kutoka,” amesema.
Amesema kutokana na hali hiyo utafika wakati maamuzi magumu yatafanyika ikiwemo kumwondoa mzabuni aliyepewa tenda ya kuzoa taka katika kata ya Ruanda na maeneo mengine yatakayobainika kukithiri kwa uchafu.
“Madiwani na wenyeviti wa Serikali za Mitaa, sisi tunapigiwa kura na wananchi, watendaji wanateuliwa, sasa umefika wakati kila tukiamka asubuhi tuangalie maeneo yetu na kama kuna uchafu tuwe wa kwanza kuokota na kuwachukulia hatua wananchi wanaotupa ovyo taka maeneo yasiyo rasmi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dk Tulia amemuagiza ofisa usafi jiji, Nimrod Kiporoza kuanza leo Jumatatu Januari 2, 2023 kutokwenda ofisini mpaka akague maeneo yote ya jiji kujiridhisha hali ya usafi ilivyo na endapo kama kutakuwa na sababu ya magari atoe taarifa.
“Mkurugenzi Jiji, ofisa usafi jiji usimpangie majukumu mengine kuanzia leo, mwache afuatilie suala la usafi ili jiji liwe na hadhi ya kuitwa jiji,” amesema.
Diwani kata ya Ruanda jijini hapa, Reuben Kipalule amesema hali hiyo imetokana na uwezo mdogo wa mzabuni aliyepewa tenda ya kutoa taka katika eneo ambalo sio rasmi.
“Mimi huyu mzabuni nilimpinga kwenye vikao lakini wenzangu waliniona kama nina chuki naye na ndiyo majibu haya yanaonekana hapa leo, cha msingi Spika, maguba yaondolewe katika eneo hilo sambamba na kutafuta wazabuni wengune watatu kutokana na ukubwa wa kata hii,” amesema.
Naibu meya wa jiji la Mbeya, Kefasi Mwasote amekiri jiji limekithiri kwa uchafu na kumueleza Spika, Dk Tulia baada ya kutoka hapo watafanya kikao na wenyeviti wa Serikali za Mitaa na madiwani wote.
“Nikiri hali sio nzuri na leo ilikuwa sio jukumu lako kuja kufanya usafi ila niombe wenyeviti wa Serikali za mitaa watanivumilia kwa maamuzi ambayo tutayachukua dhidi yao,” amesema.
Kaimu mkurugenzi wa jiji, Triphonia Kisiga ameomba radhi na kwamba hali hiyo haitojirudia licha ya makusanyo ya ada ya taka kukusanywa na watendaji wa kata kwa kushirikiana na wananchi.
“Kwa mwezi kila kata inakusanya zaidi ya Sh9 milioni fedha ambazo haziingizwi jiji, sasa tunashindwa kuelewa nini sababu ya mitaa na kata kuwa katika hali ya uchafu,” amesema.
Mkazi wa Ruanda Jijini hapa, Salina John amesema kuwa wako hatarini kuugua magonjwa ya milipuko kutokana na kuzaliana kwa wadudu ikiwepo nzi na funza