Dodoma wapewa kanuni tatu kujikinga na corona.

  • Mkuu wa mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka akigawa barakoa kwa kikundi cha ngoma cha JKT Makutupora.

Muktasari:

  • Mkuu huyo wa mkoa amesema uhai wa mtu ni wa mtu mwenyewe hivyo anapaswa kujilinda mwenyewe siyo Serikali kumlinda kwani akifa Serikali itaendelea kuwepo.

Dodoma. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka ameagiza wananchi katika mkoa huu kutembelea kwa kutumia kanuni tatu ili waweze kuokoa maisha yao.

Kanuni hizo ni maji tiririka, vitakasa mikono na kujiepusha na misongamano au kuvaa barakoa akisema ugonjwa wa korona hasa awamu ya tatu hali yake si nzuri kwa sasa.

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi kwenye siku ya PASS Trust ambayo imefungwa na Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda baada ya maonyesho ya wiki moja.

Mtaka amesema uhai wa mtu unapaswa kulindwa na mtu mwenyewe hivyo Serikali imemaliza kazi yake ambayo ni kutoa taarifa na kuwakumbusha tu.

Mkuu wa mkoa ameagiza katika maeneo yenye mikusanyiko ikiwemo masokoni, stand za mabasi na maeneo yenye mikusanyiko kwamba wahusika wachukue tahadhari na kuhimizana kuwa na maji ya kunawa.

"Lakini naomba nimnukuu Askofu Bagonza kuwa uhai ni mali yako, siyo mali ya kanisa wala msikiti, ukifa wewe Serikali,msikiti au kanisa vinaendelea kama kawaida," amesema Mtaka.

Hata hivyo Mtaka amewataka viongozi katika maeneo husika kusimamia kampeni hiyo hasa wananchi wanapoingia kwenye taasisi zao.

Kuhusu PASS Trust amewataka kuitazama Dodoma kwa nguvu zote na kwamba kila wilaya ya mkoa ichukuliwe kama eneo la mkoa ili wawekeze katika kuwasaidia wakulima.

Kiongozi huyo amesisitiza wakulima wa Dodoma kuchamkia fursa kwa kulima mazao mbalimbali yenye tija hasa zabibu ambalo ni zao pekee linalolimwa mkoani hapa.