Duni: Tunatarajia uchaguzi wa Konde utakuwa huru na haki

Thursday October 07 2021
dunipic

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Juma Haji Duni(kushoto), akimnadi kwa wananchi mgombea wa chama hicho, Mohamed Said Issa wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa marudio Jimbo la Konde uliofanyika uwanja wa Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba. Picha na Jesse Mikofu

By Jesse Mikofu

Pemba.Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT - Wazalendo, Juma Duni Haji amesema wanategemea uchaguzi wa marudio wa Konde utakuwa huru na haki tofauti na chaguzi zingine zilizotangulia.

Duni ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Oktoba 7, 2021, katika mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa marudio Jimbo la Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba, huku akisema hana cha kupoteza katika maisha yake zaidi ya kutetea haki za Wazanzibar.

Uchaguzi huo wa marudio utafanyika Jumamosi Oktoba 9, mwaka huu. Uchaguzi unafanyika kwa mara nyingine baada ya aliyechaguliwa Julai 18, mwaka huu, kwenye uchaguzi mdogo, Sheha Faki Mpemba (CCM), kujiuzulu kabla ya kuapishwa kwa madai ya familia yake kupata vitisho kutoka kwa watu aliodai ni wapinzani wake.

Hata hivyo, baadaye Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud alifichua siri kwamba chama hicho kiliwafuata Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Hussein Mwinyi kuwaeleza dhuluma iliyofanyika katika uchaguzi huo.

"Uchaguzi huu upo mikononi mwa NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi), ukiharibika wawe tayari kubeba dhamana, na safari hii hatupo tayari kudhulumiwa. Sina cha kupoteza zaidi katika maisha isipokuwa kulinda haki za Wazanzibari," amesema Duni.

Ametaka Wanachi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kumchagua mgombea wa chama hicho, Mohamed Said Issa.

Advertisement

Amezitaka mamlaka zinazohusika na usimamizi wa uchaguzi huo kuwa waungwana kwa kufuata misingi ya haki, kanuni na sheria za uchaguzi.

Naye Mwenyekiti ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo Taifa, Abdul Nondo amewataka wananchi kumchagua kiongozi wanayeona anawafaa badla ya kuchagua kwa shinikizo.

Meneja wa kampeni, Hamad Yusuf Mussa amesema, "wanawake siku ya uchaguzi amkeni mapema mkapige kura kisha mrudi nyumbani ndipo vijana na wanaume nao waende kupiga kura na wakimaliza wakae mita 100 kulinda kura hizo.

Mgombea wa jimbo hilo, Issa amesema iwapo atachaguliwa kuongoza jimbo hilo, atahakikisha anashirikiana nao kuleta maendeleo kwa watu. Amesema atashirikiana na Serikali kuboresha sekta afya, elimu na miundombinu ya barabara.


Advertisement