Edo Kumwembe : Mikono miwili ya Abramovich ilivyomchana Frank Lampard

Saturday January 30 2021
nyuma pazia pic
By Edo Kumwembe

INAWEZEKANA alikuwa amekaa ndani ya boti lake la kifahari (yatch) lenye thamani ya Dola 200 milioni. Inawezekana alikuwa amekaa katika jumba lake jipya lenye thamani ya Dola 65 milioni eneo la Herzliya nchini Israel anakoishi kwa sasa.

Jumatatu tajiri anayeitwa Roman Abramovich aliamua kuchukua moja kati ya maamuzi magumu aliyowahi kuyafanya tangu ajihusishe moja kwa moja na soka. Au unaweza kusema tangu alipoinunua Chelsea mwaka 2003.

Aliamua kumfukuza kazi kocha wake ambaye ni staa wa zamani wa timu hiyo, Frank Lampard. Kuna wachezaji wachache wa zamani wa Chelsea wanaopendwa kuliko Lampard. Na kwa kizazi kipya cha Chelsea sidhani kama kuna mchezaji aliyependwa kama Lampard. John Terry? Labda. Didier Drogba? Labda.

Lakini Roman ameamua kuchukua maamuzi haya dhidi ya mtu ambaye ni rafiki yake wa karibu. Mtu ambaye akiwa ni mchezaji, huku yeye akiwa ni tajiri bado aliweza kumkaribisha katika Yatch yake na wakanywa pombe pamoja.

Ni maamuzi mazito. Mwanamuziki mmoja wa kizazi kipya wa Tanzania, Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’ aliwahi kusema ‘Ni kazi chafu lakini lazima mtu aifanye’. Roman ameifanya huku sura yake ikitiririka machozi. Laptop yake ilikuwa ikitiririka machozi wakati akichukua maamuzi haya.

Lampard ndiye mfungaji bora wa muda wote Chelsea akiwa na mabao 211. Kumbuka aliyafunga haya akiwa kiungo. Lampard ni miongoni mwa wachezaji tisa tu ambao wamefunga zaidi ya mabao 150 katika Ligi Kuu ya England. Na katika orodha hii yeye ndiye kiungo pekee.

Advertisement

Ameichezea Chelsea kwa miaka 13, huku yeye na mastaa wengine wachache klabuni wakiwa alama zaidi kwa mashabiki na nembo ya klabu. Ukienda pale Stamford Bridge kuna mabango yao. Wao ni miungu watu. Lakini Roman amelazimika kuifanya kazi hii chafu ya kumuondoa klabuni huku akitoa machozi.

Katika makocha kama 14 wa Chelsea ambao Roman amewafukuza, huyu ndiye ambaye alikuwa na uhusiano mkubwa zaidi na klabu. Haishangazi kuona Roman aliandika ujumbe binafsi akielezea maamuzi yake ya kumtimua Frank. Hakuwahi kufanya hivyo kwa makocha wengine aliowatimua.

Kilichomponza Frank ni namna ambavyo Chelsea ilikuwa haieleweki huku Abramovich akiwa amechoma kiasi cha pauni 230 milioni kununua mastaa kibao katika dirisha moja tu la uhamisho. Hakuna timu ya England iliyochomeka kiasi hiki cha pesa kwa usajili wakati huu wa Corona. Hakuna.

Mpaka wakati Lampard anafukuzwa Chelsea ilikuwa ya tisa katika msimamo wa Ligi. Katika nafasi hii hii waliyopo, wachezaji mastaa ambao wamenunuliwa kwa bei chafu wamekuwa hawatambi. Kina Kai Havertz, Timo Werner, Hakeem Ziyechi na wengineo.

Lampard ameiacha Chelsea ikiwa imefungwa mechi sita na kutoka sare tano. Hiki si kitu ambacho Abramovich alikitazamia baada ya kutumbukiza kiasi cha pauni 230 milioni katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto.

Kwa wanaomfahamu Abramovich vizuri ni wazi kwamba alichelewa kuchukua maamuzi haya. Labda kwa sababu ilikuwa inamchukua wakati mgumu kushika Laptop yake na kuandika barua pepe ya kumfukuza kazi Lampard.

Maamuzi ya Abramovich yanaacha ladha ya uchungu katika ndimi za mashabiki wa Chelsea na wale wa England kwa ujumla wao. Hawa wa Chelsea wangependa kumuona mtu wao, anayeifahamu zaidi klabu, aliyeivaa jezi yao kwa machozi, jasho na damu akifanikiwa tena kama kocha.

Ingekuwa hadithi ya kusisimua sana. Lakini kuna hadithi chache za kusisimua za namna hii. Ni nadra kwa watu wa aina hii kufanikiwa. Kwa haraka huwa anakumbukwa mtu mmoja tu aliyefanikiwa kuwa kocha mahiri katika klabu ile ile aliyoichezea kwa umahiri.

Huyu ni Johan Cruyff. Alizichezea Ajax na Barcelona kwa mafanikio na hapo hapo akaja kuwa kocha wa timu hizi mbili kwa mafanikio. Wapo pia akina Zinedine Zidane na Pep Guardiola. Hata hivyo wengine wengi tuna mifano ya kufeli tu. Lampard anaingia katika mfano huu wa kufeli kati ya mifano mingi ambayo tunayo mkononi.

Ni ndoto kumuona Thierry Henry akiifundisha Arsenal kwa mafanikio, ni ndoto kumuona Steven Gerrard akiifundisha Liverpool kwa mafanikio. Niamini mimi kwamba hizi ni ndoto za kufikirika tu. Zina asilimia nyingi ya kufeli kuliko kufaulu.

Achana na mashabiki wa Chelsea na Lampard wao, Waingereza pia wanasikitika kwa ujumla kumuona Lampard akifeli. Wangependa na wao wawe na makocha vijana ambao wangepata mafanikio katika soka katika ngazi za juu.

Wajerumani, Wahispaniola, Wafaransa na Waitaliano wamekuwa wakizalisha makocha wa kujivunia katika miaka ya karibuni. Makocha hawa wamekuwa wakipata mafanikio makubwa katika timu za taifa au vilabu. Hadithi hii haipo kwa Waingereza.

Wachukulie makocha kama kina Pep Guardiola, Zinedine Zidane, Julian Naggelsmann, Thomas Tuchel, Joachim Lowe na wengineo. Waingereza hawana makocha wa namna hii kwa sasa. Wanawategemea hawa hawa kina Lampard, Terry, Gerrard waibuke kukiokoa kizazi chao.

Kumbuka kuwa kina Sam Allardyce na Steve Bruce wanapitwa na wakati. Na hata kabla ya kupitwa na wakati walikuwa hawajaonyesha jambo lolote la ajabu. Hawakuwahi kuwa makocha wa timu kubwa. Hawa kina Lampard walikuwa wanatazamiwa kuingia katika kizazi cha kina Pep na kufuata nyendo zao.

Ni huzuni lakini Abramovich hakuwa na jinsi. Katika msimu wa kwanza alimvumilia Lampard kutokana na ukweli kwamba Chelsea walikuwa wamefungiwa wasisajili wachezaji. Kila mtu alijua kwamba Lampard asingeweza kutoboa katika msimu huo.

Lakini msimu huu ulikuwa wa kufa au kupona kwa Lampard. Hauwezi kusema ameonewa kwa sababu kuna makocha wengi waliofukuzwa kama yeye. Huwa inatajwa kwamba mikono miwili ya Abramovich huwa inashika vitu viwili vyenye hisia tofauti.

Mkono wa kwanza huwa unashika kitabu cha hundi kwa ajili ya kusaini mastaa wa kukitia nguvu kikosi chake, mkono wa pili huwa unashika panga kwa ajili ya kuwakata makocha waliopewa nafasi ya kuwaunganisha mastaa hao. Kwa Lampard, Roman amefanya kazi zote mbili kwa ufasaha.

Advertisement