Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

El-Nino, Hidaya zilivyoacha kilio, kicheko

Daraja la Nambilanje katika Mto Mbwemkuru linaloungnisha wilaya za Ruangwa na Kilwa  mkoani Lindi ambalo limekatika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikagua  uharibufu uliotokea katika daraja hilo, Mei 25, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Muktasari:

  • Kimbuka Hidaya kilichopita Tanzania, kuanzia Mei 12, 2024 na kudumu kwa siku takribani mbili pamoja na mvua kubwa za El nino zilizonyesha na kuharibu miundombinu mbalimbali, imekuwa fursa na maumivu kwa wananchi hasa mkoani Lindi.

Dar es Salaam. Mvua kubwa ya El nino iliyonyesha nchini na kimbunga Hidaya kilichopita mwezi huu, kimeacha kilio na maumivu mkoani Lindi sambamba na kuibua fursa ya kujipatia fedha kwa baadhi ya watu.

Mvua hizo, zilisababisha baadhi ya barabara na madaraja kusombwa na maji na kuibua kero ya usafiri kwenye baadhi ya maeneo kutokana na magari kusimamisha shughuli za kusafirisha abiria.

Hali hiyo ilifanya hata usafirishaji wa bidhaa kuwa wa tabu kwani kuna baadhi ya sehemu gharama za usafirishaji zilikuwa mara mbili.

Mwananchi ilitembelea katika baadhi ya maeneo ambayo yanafanyiwa matengenezo na Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) baada ya kuathiriwa na mvua na kuzungumza na wakazi wake.

Moja ya maeneo ambayo yalitembelewa ni daraja lililopo katika Kijiji cha Nambilanje katika Mto Mbwemkuru lililoharibiwa na mafuriko.

Daraja hili ni sehemu ya barabara ya Kiranjeranje hadi Ruangwa ambayo imeathiriwa na mvua na kusimamisha shughuli za usafirishaji abiria na mizigo.

Katika mto huo, vyombo vya moto haviwezi kupita, mitumbwi ndiyo hutumika kuvusha watu, huku pikipiki na mizigo huvushwa kwa kubebwa baada ya kushushwa kwenye gari upande mmoja na kupelekwa mwingine.

Vijana waliochukulia kadhia hiyo kama fursa wakivusha watu na mizigo katika eneo hilo, wameiambia Mwananchi kuwa  pikipiki huvushwa kwa kati ya Sh4,000 na Sh5,000.

“Ikiwa Sh4,000 tunagawana kila mmoja Sh1000 sasa kwa siku inategemeana utavusha pikipiki ngapi, haukosi kitu,” amesema Mohammed Ngonyani mkazi wa eneo la Nambilanje.

Mbali na pikipiki pia mtumbwi hutumika kuvusha watu wanaoogopa kuloana kwa Sh1,000 huku baadhi ya wananchi wakilazimika kuvua suruali zao na viatu kushika mkononi ili wavuke mto huo na kwenda upande wa pili.

Hali hii inaongeza maumivu kwa wafanyabiashara ambao wanasafirisha mizigo yao kutoka Ruangwa kuja wilaya ya Kilwa, kwani wafikapo eneo hilo hulazimika kutafuta namna ya kusafirisha mizigo yao kwenda katika vijiji walivyokusudia. Hapo vijana hao hupata fursa nyingine ya kubeba mizigo hiyo kwa kichwa na kuifikisha ng’ambo ya mto.

 “Tunaomba Serikali itutengenezee hizi barabara, zirejee katika hali yake ya kawaida, hivi tunaumia, tunasafirisha mzigo kwa gharama kubwa mwisho wa siku watakaoumia ni wananchi kwa sababu sisi tutaangalia namna ya kupunguza hasara,” amesema Richard Masawe.


Maumivu ya usafiri

Mbali na usafirishaji bidhaa, kwa wananchi ambapo ndiyo watumiaji wa barabara hiyo ikiwemo wale wa Kijiji cha Nanjirinjiri, walitaka Serikali kufanya kila liwezekanalo ili hali irudi kama kawaida.

Vijana wakivusha pikipiki  katika mto Mbwemkuru linalounganisha wilaya za Ruangwa na Kilwa  mkoani Lindi ambalo limekatika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikagua  uharibufu uliotokea katika daraja hilo, Mei 25, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

“Sasa hivi tuko kama kisiwa, ukitaka kwenda mjini (Lindi) au Dar es Salaam lazima ujipange kikamilifu unahitaji si chini ya Sh60,000 ambapo kati ya hiyo Sh40,000 au Sh50,000 utalipia bodaboda hadi sehemu unayoweza kupata usafiri,” amesema Hamida Rashid.

Hali hiyo pia ipo kwa wakazi wanaotumia barabara ya Tingi hadi Kipatimo ambao nao wanalia na maumivu ya kuongezeka kwa gharama za usafirishaji, huku kwa madereva  bodaboda ikiwa ni kicheko.

Abdul Matembo aliitaka Tanroads kuongeza nguvu ili barabara hiyo yenye urefu wa zaidi ya kilomita 40 ipitike kirahisi.

Amesema tangu kuharibika kwake kufuatia mvua za El nino na kimbunga Hidaya, gari zote zilizokuwa zikifanya safari kati ya Dar es Salaam hadi Kipatimo zilisitisha shughuli zake jambo ambalo liliongeza gharama kwa wananchi.

“Kwa gari kutoka Dar es Salaam hadi Kipatimo ilikiwa kati ya Sh18,000 hadi Sh20,000 lakini sasa hivi bila Sh70,000 haufiki, kwa sababu gari zote zinaishi Tingi, bodaboda kutoka pale zinaanzia Sh40,000 ukionewa huruma na ukijieleza,” amesema Matembo.

Francis Ngonyani naye alikazia suala hilo huku akieleza namna ilivyowaathiri katika usafirishaji bidhaa hasa nazi.

“Huku tuna nazi nyingi, mwanzoni ulikiwa ukibeba kwenye gari unatozwa kila nazi Sh100 hadi 200 hadi unapofika mjini (Dar es Salaam) lakini sasa hivi kuzitoa tu nazi huku kufika sehemu unayoweza kupata basi ya kwenda jijini Dar es Salaam unalipa hadi Sh50,000 ya bodaboda unadhani nikifikisha mjini nitauzaje,” amesema na kuhoji Matembo.

Mwajuma Haji anasema hali ilivyo sasa imewafanya kuwa kama wakazi wa kisiwani kutokana na kufika katika maeneo yao kuwa wa tabu.

“Hiyo pikipiki yenyewe ukipanda unakuwa na hofu muda wote, Mungu asaidie wamalize matengenezo kwa wakati,” amesema Mwajuma.


Bodaboda wachekelea

Wakati wananchi  wakiyasema hayo, Bodaboda eneo hilo wanasema tangu kuwapo kwa athari hizo imekuwa neema kwao kutokana na kujiingizia fedha nyingi katika usafirishaji bidhaa.

“Mbali na abiria tunasafirisha sana mizigo ikiwemo nazi, gunia moja ni kati ya Sh30,000 hadi Sh50,000 kulingana na umbali hadi kufika hapa unapoweza kupata usafiri wa kwenda unakohitaji, kwa siku ukienda mara mbili mara tatu si haba,” amesema Jafari Masanja ambaye ni bodaboda na mkazi wa Mingumbi.

Hofu ya Saida Waziri iko juu ya akinamama wanaohitaji huduma za dharura inapobidi kusafiri kwani bodaboda pekee ndiyo inaweza kutumika.

“Na hiyo bodaboda si kwamba mtasafiri tu moja kwa moja kuna maeneo hayapitiki kirahisi, hili linaongeza muda wa kufikia huduma za afya katika hospitali za wilaya,” amesema Saida.


Ujenzi waanza

Barabara ya Tingi – Kipatimo, tayari mkandarasi ameshaanza kufanya marekebisho ikiwa ni baada ya kusaini mkataba Machi mwaka huu, lakini awali mvua ilikuwa kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mkurugenzi wa kampuni ya Mucadamu and Sons, Kasmir Mucadam amesema kusimama kwa mvua sasa kutafanya shughuli hiyo kufanyika kwa wepesi.

Akizungumzia suala hilo, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Lindi, Emil Zengo amesema tayari kambi maalumu imewekwa na wataalamu wake kuhakikisha mawasiliano ya Kipatimo yanarejea.

“Eneo la kwanza lililokarabatiwa ni kujaza kifusi katika daraja lililokuwa limebebwa na maji lililopo katika kijiji cha Mingumbi ikiwa umbali wa kilomita 12.5 kutoka Tingi ilipo barabara kuu ya Dar es Salaam kwenda Mtwara. Kujazwa kifusi katika eneo hilo la daraja sasa kutaruhusu ujenzi kuendelea katika maeneo mengine ya mbele hadi watakapomaliza,” amesema Zengo.

Kuhusu barabara inayounganisha wilaya ya Kilwa na Raungwa, Zengo amesema ina umuhimu mkubwa kwa watu wa Ruangwa na maeneo jirani ikiwemo Nanjirinji kwani ni wakulima wazuri wa ufuta, mbaazi na hata uchimbaji wa madini mbalimbali.

“Mvua za El- Nino zilibeba daraja katika mto Mbwemkuru na kukata mawasiliano kati ya Namichiga na Kiranjeranje, huku nako tumeweka kambi ambayo itakuwa kubwa na tunaiomba Serikali kutuongezea nguvu ili kuhakikisha barabara zote zinapitika muda wote,” amesema Zengo.

Amesema kwa sasa barabara hiyo ina maeneo ambayo mvua zinaponyesha yanajaa maji na mengine  yanahitaji kujengwa madaraja huku akieleza kuwa bajeti ya Serikali itakaporuhusu kama Tanroads watakuwa tayari kujenga miundombinu ya makaravati na madaraja, ili barabara hii iweze kutumika muda wote.

Kufanya hivyo kutasaidia kuunganisha wilaya ya Kilwa na Ruangwa na kuwawezesha wananchi kusafirisha mazao yao na kupata chakula ambacho hawawezi kulima

“Pia waweze kusafirisha madini mbalimbali ambayo yanapatikana kwa wingi sana katika eneo hili, kwa kuzingatia hayo sisi  Tanroads Lindi tuko tayari kusimamia matengenezo yanayohitajika ya muda mfupi na mrefu,” amesema Zengo.


Ziara ya Majaliwa

Siku chache baada ya ziara ya Tanroads katika eneo hilo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa juzi alifika ili kujionea hali halisi huku akieleza Serikali imejipanga kuhakikisha inarejesha mawasiliano yote yaliyoathiriwa na mvua.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Wananchi wakati alipokagua  daraja la Nambilanje  katika mto Mbwemkuru linaloungnisha wilaya za Ruangwa na Kilwa  mkoani Lindi, Mei 25, 2024. Daraja hilo limekatika kutokana mvua kubwa zilizonyesha. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

“Kwa bahati nzuri Tanroads wameshafika wameangalia hii hali na Waziri wa ujenzi wa ujenzi (Innocent Bashungwa) amekuja kutoa taarifa kwangu na mbunge mwenzangu wa Kilwa kusini kuwa Tanroads wanaendelea na uhakiki wa namna watakavyorejesha miundombinu hii,” alisema Majaliwa.

Aliwataka wananchi kuwa watulivu kwani taarifa za hali ya hewa zinaonyesha kuwa mvua itaendelea kunyesha na kinachosubiri ni taarifa hizo kueleza inaelekea kuisha ili tathmini ifanywe kwenye barabara zote za vijijini, zinazounganisha kata na kata, wilaya na barabara kuu.

“Baada ya kufanya tathmini Serikali itatoa fedha na kutangaza zabuni za ujenzi wa njia zenyewe, madaraja na makaravati ambayo yanahitaji kurejeshwa katika hali yake ya kawaida,” alisema Majaliwa.

Majaliwa alisema eneo hilo ni miongoni mwa miradi mikubwa ambayo anakwenda kuisimamia ndani ya Serikali na kuiomba Serikali kuwekeza katika ujenzi wa daraja hilo refu.